Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitaka klabu ya Yanga kuwasilisha rasimu ya
Katiba waliyoipitisha, kwa kuzingatia kuwa Muhtasari wa kikao cha Mkutano Mkuu
wao wa Juni 1 mwaka huu umeainisha baadhi ya marekebisho waliyofanya kwa
tulivyowaelekeza.
Yanga
wanatakiwa kuwasilisha rasimu hiyo kabla ya Oktoba 5 mwaka huu. Ikiwa
itakubaliwa na TFF, itapelekwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo ili
waweze kufanya uchaguzi wa viongozi wao.
TFF KUCHUNGUZA
HUJUMA DHIDI YA STARS
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa
zilizoandikwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari zikielezea tuhuma za hujuma
kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi za kufuzu mashindano ya AFCON.
TFF pamoja na kutokuwa na uthibitisho
wa tuhuma hizi nzito haliwezi kuzikalia kimya. Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania litateua jopo la kuchunguza tuhuma hizi.
Wanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania
(Members of TFF Family) watakaohitajika kuhojiwa na jopo hilo kwa mujibu wa
Ibara ya 37 ya Kanuni za Maadili za TFF watalazimika kutoa ushirikiano.
Atakayeshindwa kutoa ushirikiano atachukuliwa hatua za kimaadili.
Pia wadau wa mpira wa miguu ambao sio
wanafamilia wa TFF, watakaoitwa na jopo hili wanaombwa watoe ushirikiano kwa
nia ya kujenga mpira wetu.
KATIBU
COASTAL UNION KUPELEKWA MAADILI
Katibu Mkuu wa
Coastal Union, Kassim El Siagi atafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushinikiza mkutano wa wanachama wa klabu
hiyo ufanyike bila kuandaliwa na Kamati ya Utendaji.
Pia El Siagi
alitumia vyombo vya habari kuishambulia TFF ambayo haikutambua uamuzi wa
mkutano huo ulioelezwa kumdumaza Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Steven Mnguto.
TFF ilimtuma Mkurugenzi
wake Msaidizi wa Sheria na Uanachama kufanya uchunguzi wa mgogoro uliokuwa unaendelea
katika klabu hiyo.
Baada ya
kupokea taarifa ya uchunguzi huo, TFF imebaini kuwa Mwenyekiti na Mweka Hazina
wa klabu hiyo walishajiuzulu, hivyo uitishwe uchaguzi haraka na kujaza nafasi
hizo na nyingine zilizo wazi.
Pia wajumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Coastal Union, Salim Amir na Albert Peter wameonywa kwa
kushiriki katika mkutano ambao wanajua haukuandaliwa na Kamati ya Utendaji.
Vilevile
uchunguzi wa TFF umebaini kuwa ushiriki wa Salim Bawazir na Akida Machai kwenye
vikao vya Kamati ya Utendaji ya Coastal Union si halali kwa vile wajumbe wa
kamati hiyo wanachaguliwa na Mkutano Mkuu na si kuteuliwa na Mwenyekiti.
Kwa vile kutakuwa
na uchaguzi wa kujaza nafasi ambazo zipo wazi, uchaguzi huo utasimamiwa na
Kamati ya Uchaguzi ya Coastal Union kwa kushirikiana na Kamati ya Uchaguzi ya
TFF, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga na Coastal Union watafanya
uhakiki wa reja ya wanachama.
BONIFACE
WAMBURA
KNY
KATIBU MKUU
SHIRIKISHO
LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment