Kijana wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoani Ruvuma
Mustafa Hamad Mlanzi akimfunga skafu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi mara tu baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa
Songea kuanza ziara ya siku mbili Mkoani humo kukagua miradi ya
maendeleo.
Balozi Seif akisalimiana na baadhi ya Viongozi wa
Serikali na Kisiasa mara baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa
Songea.
Kikundi cha Utamaduni ya Shaba Sanaa cha Songea
kikiimba wimbo maarufu wa Lisombe kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Songea kwa ziara ya siku
mbili Mkoani Ruvuma.
Mbunge wa Jimbo la Paramelo Mh. Jenista Mhagama
akimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa kukubali
kwake kufanya ziara Mkoani Ruvuma.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewasili Mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku mbili kuangalia miradi mbali mbali ya kiuchumi na maendeleo ya Mkoa huo kwa mualiko wa Uongozi wa Jimbo la Peramilo.
Kwenye uwanja wa ndege wa Songea Balozi Seif na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi akiambatana pia na Wake wa wabunge na wawakilishi Zanzibar alilakiwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mpya wa Njombe Mh. Aseri Msangi pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali na Siasa.
Akitoa Taarifa fupi ya Mkoa huo mara baada ya mapokezi hayo hapo Ikulu ya Mkoa wa Ruvuma Kaimu Mkuu wa Mkoa huo Mh. Aseri Msangi alisema Mkoa wa Ruvuma umekuwa na mafanikio makubwa ya sekta ya kilimo kwa kubarikiwa kuwa na mvua za kutosha.
Mh. Msangi alisema Msimu huu wa kilimo Mkoa wa Ruvuma umezalisha tani Milioni Moja nukta nne za chakula ukiwa na ongezeko la ziada ya Tani Laki Tisa ikiwa ni sawa na Asilimia 10.2%.
Alisema mafanikio hayo yamesababisha changamoto kubwa la uhifadhi wa nafaka kutokana na uhaba wa maghala pamoja na uchelewaji wa fedha za ununuzi wa Mahindi kutoka kwa wakulima.
Hata hivyo Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvuma aliwahakikishia wakulima waliouza mahindi yao ambao bado hawajapata fedha zao kwamba Serikali imeshatenga fedha hizo zinazotarajiwa kuwafikia wakati wowote kuanzia sasa.
Akigusia huduma za maendeleo na kiuchumi Mh. Msangi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Ruvuma imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia mipango ya kiuchumi ili kutekeleza sera na ilani ya CCM ya mwaka 2010.
Alisema mipango hiyo iliyojikita zaidi katika miradi ya kiuchumi na ustawi wa jamii imelenga kwenda sambamba na Dira ya Taifa iliyokusudia kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati na kati ifikapo mwaka 2025.
Kuhusu sekta ya afya Mh. Aseri Msangi alifahamisha kwamba Mkoa wa Ruvuma umefikia kuwa na vituo vya afya 271 kukiwa na ongezaeko la zaidi ya asilimia ishirini na sita.
Alisema kinachoupa mtihani Mkoa huo hivi sasa ni ongezeko la maambukizi ya virusi vya ukimwi iliyofikia asilimia 7% hali ambayo Uongozi wa Mkoa huo unatafuta mbinu za kupunguza kasi ya kuenea kwa maambukizi hayo.
Mh. Msangi alisema juhudi za ziada zitachukuliwa katika kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya hasa katika skuli zote za sekondari na msingi ili kupunguza kasi hiyo iteremke hadi kufikia asilimia 3%.
Akitoa shukrani zake kwa mapokezi hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzinbar Balozi Seif Ali Iddi alizipongeza juhudi zinazochukuliwa na Viongozi na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma katika kujiletea maendeleo yao.
Balozi Seif alisema takwimu zinaonyesha wazi kwamba Mkoa wa Ruvuma umepata mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo, afya pamoja na elimu na kuwa mfano bora kwa mikoa mengine hapa nchini.
Alisema Wananchi na Jamii kote Nchini wanapaswa kumpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na juhudi anazochukuwa za kusimamia na kuhamasisha maendeleo ya umma hasa katika sekta muhimu ya Elimu.
Balozi Seif alisema muongozo wa Rais Kikwete wa kuzitaka Wilaya zote nchini kumaliza ujenzi wa madarasa ya Maabara katika skuli zote za sekondari Wilaya ifikapo Mwezi Disemba mwaka huu umeonyesha juhudi hizo za kumkomboa Mtoto wa Kitanzania ili aoane na karne hii ya sayansi na Teknolojia Duniani.
Naye Mbunge wa Jimbo la Peramilo ambaye ndie mwenyeji wa ziara hiyo Mh. Jenista Mhagama alisema ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar imeonyesha mapenzi na mshikamano uliopo kati ya pande mbili zilizounda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/10/2014.
No comments:
Post a Comment