HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 18, 2014

DK. SLAA AENDELEA KUTIKISA VIJIJNI OPERESHENI DELETE CCM

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbroad Slaa akihutubia maelfu ya wananchi wa Kijiji cha Ludewa, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro katika mkutano wa Oparesheni Delete CCM, uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ludewa juzi. (Na Mpiga Picha Wetu)
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbroad Slaa akihutubia maelfu ya wananchi wa Kijiji cha Ludewa, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro katika mkutano wa Oparesheni Delete CCM, uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ludewa juzi. (Na Mpiga Picha Wetu)


Na Mwandishi Wetu, Kilosa

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbroad Slaa ametoa kauli nzito kuhusu migogoro ya ardhi inayoendelea maeneo mbalimbali nchini na kusababisha mauaji ya kutisha, akimtaka Rais Jakaya Kikwete kumfukuza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, la sivyo wananchi wanaoona damu ikimwagika hawawezi kumwelewa.

Amewataka Watanzania wote hususan jamii za wakulima na wafugaji kuacha kupigana na kuuana wakigombea ardhi badala yake waiwajibishe Serikali ya CCM, akisisitiza kuwa migogoro hiyo ni matokeo ya serikali hiyo kushindwa kuwajibika ipasavyo hasa katika kuweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi ambayo ni majukumu ya Serikali za Mitaa.

Dkt. Slaa ambaye jana alianza ziara ya chama hicho iliyopewa jina la ‘Operesheni Delete CCM’ akimpokea Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe, amesema kuwa migogoro ya ardhi inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha umwagaji damu za Watanzania na uharibifu mkubwa wa mali ni matokeo ya kushindwa kwa sera, mipango na mikakati ya CCM, hivyo akawataka wananchi kujiandaa kukipumzisha chama hicho kutoka madarakani.

Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza kijijini Mvuha, kati ya mikutano mitano kwenye vijiji mbalimbali vya majimbo ya Morogoro Kusini, Morogoro Kaskazini na Kilosa, Dkt. Slaa alisema kuwa umwagikaji wa damu huo usipodhibitiwa na migogoro hiyo kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu, Serikali itakuwa imeshindwa moja ya majukumu yake ya msingi, kulinda raia wake.

“Ndugu zangu ziara hii itanifikishakatika maeneo ambayo mnajua yamekuwa na migogoro ya ardhi…kumekuwepo na migogoro hata huku kwenu isiyokwisha ya wakulima na wafugaji kugombea ardhi…Mkoa wa Morogoro baraka ya ardhi na utajiri wa rutuba mliopewa umekuwa ukigeuka laana kiasi cha damu za watu kumwagika.

“Yanatokea sana huko Mvomero, Kilosa hata hapa kwenu (Mvuha) nimeambiwa migogoro ipo. Tunavyozungumza hivi sasa kuna matukio ya kutisha yametokea huko Kiteto, Siha, Malinyi na kwingine. Ndugu zangu, wakulima na wafugaji…ninyi wote ni Watanzania. Nawaomba sana muendelee kuishi kama ndugu kama ilivyokuwa huko nyuma.

“Haya ni matokeo ya Serikali kushindwa majukumu yake. Ni matokeo ya sera za CCM kushindwa. Mipango na matumizi mazuri ya ardhi, ili ardhi ya mifugo ijulikane na ardhi ya kilimo ijulikane na matumizi mengine ni kazi za Serikali za Mitaa kupitia halmashauri. Huko kote sera za CCM zimeshindwa. Ndiyo maana tunasema delete CCM,” alisema Dkt. Slaa na kuongeza;

“Kupitia mkutano wangu huu leo tunaitaka Serikali ya Kikwete ichukue hatua za haraka sana kuzuia umwagaji wa damu unaoendelea na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi nchini. Vinginevyo wanazidi kudhihirisha kuwa wamechoka na watakiwa kupumzishwa.

“Kwa Kiteto mojawapo ya chanzo cha mauaji yanayoendelea huko ni wanasiasa wanaoongoza wilayani humo, akiwemo Mkuu wa Wilaya, yuko Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, yupo mbunge wa jimbo ambaye amewahi kuwa waziri…mgawanyo wa ardhi ni jukumu la serikali. Hatuwezi kuangalia tu damu ya Watanzania inamwagika kama kuku. Hatuwezi. Tunamtaka Kikwete amfukuze kazi huyo DC,” alisema Dkt. Slaa.

Aliongeza kusema kuwa iwapo viongozi walioko madarakani sasa hawataona thamani za damu zinazomwagika kwa sababu ya wao kushindwa kutekeleza wajibu wao, iko siku watailipa kwa gharama kubwa endapo wananchi wataendelea kupoteza matumaini huku haki ikiwa haipatikani, huku akisisitiza kuwa hayo yataanza kuonekana kuanzia uchaguzi wa Desemba 14 mwaka huu.

Dk. Slaa ambaye jana alifanya mikutano katika vijiji vya Mvuha, Kisika, Ludewa, Magubike na akimaliza mkoa wa Morogoro na leo anaingia mkoani Dodoma, aliwataka Watanzania katika jamii zao, zikiwemo za wakulima na wafugaji, kuacha kuuana wao kwa wao, badala yake wajue namna ya kushughulikia chanzo cha migogoro yao, amabacho alidai ni serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.

No comments:

Post a Comment

Pages