HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

July 07, 2026

AZANIA BANK YAENZI USHINDI WA RIADHA DAR MASHINDANO YA TAIFA

BENKI ya Azania, imeipongeza timu ya Riadha ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushika nafasi ya pili katika Mashindano ya Taifa 'National Athletics Championship' yaliyofanyika viwanja vya Filbert Schools Mkuza Kibaha mkoani Pwani Julai 3-4 mwaka huu.

Azania Bank imefungua milango ya mashirikiano na Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam ( DAA), ambapo ilidhamini vifaa vya michezo kwa timu hiyo wakati ikienda kushiriki mashindano hayo.



Katika hafla ya kuiaga timu hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Julai 2, Meneja wa Benki ya Azania Tawi la Lumumba, Valentina Chasama, aliwaasa wachezaji hao kwenda kujituma na kuhakikisha wanarejea na ushindi, na Azania Bank itawapokea kwa kishindo.

Mbali na Chasama, Mgeni rasmi katika hafla hiyo Ofisa Utamaduni Manispaa ya Temeke, Kasim Semfuko, na Diwani wa Kata ya Azimio Temeke, Hamduni Mohamed Ally 'Saddam', pia  waliwataka vijana hao kuupambania Mkoa wa Dar es Salaam huku nidhamu ikiwa ndio nguzo yao kuu.

Katika mashindano hayo yaliyoshirikisha mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani, Mjini Magharibi waliibuka mabingwa wakifuatiwa na Dar es Salaam huku nafasi ya tatu ikienda kwa Kusini Unguja.

Mara baada ya kurejea jijini timu hiyo Julai 5, Julai 6 msafara wa wachezaji na viongozi ulitembelea Tawi la Azania Bank Lumumba na kupokewa na Meneja, Valentina Chasama.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, Nahodha wa timu hiyo, Mpaji Gibdon, alisema udhamini wa Azania Bank uliwapa hamasa ya kwenda kujituma na kutekeleza maagizo waliyopewa na wanashukuru Mungu, wamelifanikisha kwa asilimia 99.

Naye Kocha wa timu hiyo Erick Magesa, aliishukuru Azania Bank kwa kuwapamba, jambo lililowafanya kuonekana wakipekee katika mashindano hayo, jambo lililowaongezea hamasa ya kujituma zaidi.

Magesa, pia aliupongeza uongozi wa DAA, kwa mabadiliko makubwa ya kiutendaji wanayoendelea kuyafanya katika kukuza vipaji vya riadha Dar es Salaam.

Naye Mwenyekiti wa DAA, Amani Mnkande Ngoka, aliishukuru Azania Bank, na kwamba kilichofanywa na timu hiyo mwaka huu hakijawahi kufanywa kwa zaidi ya miaka 11 na kuahidi mwakani wanalenga kukamata nafasi ya kwanza kabisa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Azania Bank, Meneja tawi la Lumumba, Chasama, amewapongeza wachezaji kwa ushindi huo na kwamba wataendelea kuwasapoti ili wafikie na kufanikiwa kitaifa na kimataifa.

Chasama, amesema Azania Bank imetekeleza ahadi na ndio maana imewapokea wachezaji na viongozi wa timu hiyo, na kila mmoja amefunguliwa akaunti na itawekwa zawadi zao.

Meneja huyo, amesema kwa sasa Azania Bank imefungua rasmi mashirikiano endelevu na Riadha Dar na itaendelea kusapoti programu mbalimbali za maendeleo ya riadha zinazoendeshwa na DAA.


No comments:

Post a Comment

Pages