Ofisa Wakala wa Nje kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
PPF, Pima Mohamed akitoa maelezo ya huduma zinazotolewa na mfuko huo kwa Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa (katikati) alipotembelea banda hilo
wakati wa ufunguzi wa Kampeni ya Mwanamke na Uchumi iliyofanyika jijini
Tanga na kuandaliwa na Kampuni ya Angels
Moment. Kulia ni Mkurungenzi wa kampuni hiyo, Naima Malima. (Picha na Elizabeth Kilindi)
NA ELIZABETH KILINDI, TANGA
WANAWAKE wajasiriamali Mkoani Tanga wametakiwa kuwekeza kwenye ardhi ili kuweza kujikwamua kiuchumi kwani kilimo ni mkombozi katika kuinua uchumi.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Chiku Gallawa wakati wa semina ya kampeni ya mwanamke na uchumi iliyoandaliwa na kampuni Angels Moment katika ukumbi wa Naivera ambapo alitolea mfano katiba ya sasa ambayo imetoa kipaumbele cha mwanamke kumiliki Ardhi.
Mkuu wa Mkoa huyo alisema wanawake wamekuwa wakijishughulisha na na shughuli mbalimbali za mikono lakini zimekuwa haziwaletei maendeleo ya haraka.
‘Wajasiriamali wa Tanga wanafanya shughuli nyingi za mikono lakini maendeleo hayatokei kwa haraka na hivyo nawaomba nunueni Ardhi ambayo ni kitu cha kudumu na kilimo hakimtupi mtu hata siku moja’ alisema Gallawa.
Hata hivyo aliongeza kuwa shughuli za ujasiriamali ziungwe Mkono na kuhakikisha zinafanyika katika mazingira rafiki yatakayomsaidia
mwanamke.
Nae Mkurugenzi wa Kampeni ya wanawake na uchumi Mahada Erick alisema wanawake wajariamali wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa mitaji na uwezo mdogo kuzitambua fursa zilizopo katika maeneo yao.
Aidha alisema kuwa jamii pia imekuwa ikishindwa kuwaunga mkono katika uwekezaji wa rasilimali ardhi hali ambayo inasababisha wakinamama wengi kuogopa kushiriki katika Shughuli za kilimo.
No comments:
Post a Comment