Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akitaja kikosi cha timu ya
taifa kitakachopambana na Swaziland Novemba 16 jijini Mbabane. Kulia ni
Meneja wa timu hiyo, Boniface Clemence na Mratibu wa timu za Taifa, Martin
Chacha. (Picha na Francis Dande)
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij ametangaza
kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Swaziland itakayochezwa Novemba 16
mwaka huu jijini Mbabane.
Akizungumza Dar es Salaam, leo (Novemba
5 mwaka huu), Nooij alisema kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 10 mwaka huu
saa 6 mchana kwenye hoteli ya Accomondia, na siku hiyo hiyo jioni kitafanya
mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.
Novemba 11 mwaka huu, Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka kwenda Afrika Kusini
ambapo itaweka kambi ya siku mbili kabla ya kuondoka Novemba 13 mwaka huu
kwenda Swaziland.
Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho
ni makipa Aishi Manula (Azam) na Deogratias Munishi (Yanga). Mabeki ni Abubakar
Mtiro (Kagera Sugar), Aggrey Morris (Azam), Emmanuel Simwanda (African Lyon), Hassan
Isihaka (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Osacr Joshua
(Yanga), Said Moradi (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shomari Kapombe
(Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Erasto
Nyoni (Azam), Haruna Chanongo (Simba), Himid Mao (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al
Markhiya, Qatar), Said Ndemla (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Washambuliaji ni Juma Luizio (ZESCO,
Zambia), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon
Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo).
WADAU KUBUNI JEZI MPYA YA TIMU ZA TAIFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linakaribisha
wabunifu, kubuni mwonekano wa jezi mpya za timu ya Taifa kwa mechi za nyumbani na
ugenini. Ubunifu ni lazima uzingatie rangi za bendera ya Taifa.
Mshindi wa jezi ya nyumbani atapata sh. 1,000,000 (milioni moja),
na mshindi wa jezi ya ugenini atapata pia sh. 1,000,000 (milioni moja).
Ubunifu utumwe kwenye anwani ya barua pepe: info@tff.or.tz
au uwasilishwe kwa CD au flash zikiwa katika mfumo wa PDF katika ofisi za TFF
zilizopo ghorofa ya tatu katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Ohio na Garden
Avenue. Mwisho wa kupokea designs ni Novemba 15, 2014.
Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana nasi kwa simu namba; 0713
210242 au 0714 634838.
MPANDA UTD,
UJENZI RUKWA KUANZA SDL
Michuano ya Ligi
Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 katika makundi manne ya timu sita
sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka
huu ambapo Mpanda United itakuwa mwenyeji wa Ujenzi Rukwa.
Mechi hiyo ya
kundi A itachezwa kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga. Siku hiyo hiyo
katika kundi hilo kutakuwa na mechi kati ya Mvuvumwa FC na CDA (Lake
Tanganyika, Kigoma), na Milambo dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Kundi B mechi za
ufunguzi ni kati ya Pamba na JKT Rwamkoma kwenye Uwanja wa CCM Kirumba huku
Bulyanhulu FC ikiwa mwenyeji wa AFC kwenye Uwanja wa Bulyanhulu mkoani
Shinyanga.
Abajalo FC ya
Dar es Salaam itaikaribisha Kariakoo FC ya Lindi kwenye mechi ya kundi C
itakayochezwa Uwanja wa Karume. Nazo Kiluvya United na Transit Camp
zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.
Kundi D mechi
tatu za ufunguzi ni kati ya Town Small Boys na Volcano FC (Uwanja wa Majimaji,
Songea), Njombe Mji na Mkamba Rangers (Uwanja wa Sabasaba, Njombe), na Wenda FC
dhidi ya Magereza Iringa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment