ABDALLAH NA SHEHE SEMTAWA
MJUMBE wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), Muslim Hassanali, amedai kushambuliwa na katibu kata wa
kata ya Kisutu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM),Sauda Addey, baada ya mjumbe
huyo kukataa kubandika kipeperushi cha wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa
serikali za mitaa kupitia CCM mbele ya eneo lake la biashara.
Hassanal anadai tukio hilo lilitokea juzi jumamosi
saa tano asubuhi baada ya wafuasi wa CCM kubandika kipeperushi chao katika eneo
lake la biashara lililopo mtaa wa Mali Kisutu jijini Dar esSalaam.
Kushambuliwa kwa Hassanal kumekuja ikiwa ni siku
chache zimepita huku baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa katika maeneo mbali
mbali nchini wakiwa wameshashambuliana na wengine kusabaishiwa vifo.
Akizungumzia namna alivyoshambuliwa Hassanal alisema
baada ya kufika ofisini kwake alikuta kipeperushi hicho na alipouliza watu
aliowakuta wakamuambia kuwa makarataisi hayo yamewekwa usiku na kwamba hawamjui
aliyeweka.
“Kisheria lile ni eneo langu ninalolimiliki
kibiashara hivyo yeyote anayetaka kulitumia ni lazima aonane na mimi nimpe
ruhusa ama la sasa hawa CCM wamekuja kuweka pasipo ridhaa yangu na mimi
siipendi CCM nikiona hata rangi zao nasikia kichefu chefu nikaona ngoja
niziondoe”alisema Hassanal na kuongeza.
“Unajua ile ni sehemu ya biashara wanafika watu wa
kila itikadi sasa kubandika picha kama zile zinaweza kuvuruga biashara zangu
isitoshe kwa kulitambua hilo ndio maana nimeshindwa hata kubandika picha za
wagombea wa Chadema ambacho ni chama changu”.
Alidai kuwa baada ya kuyaondoa matangazo hayo viongozi wa Kata hiyo wa CCM wakiambatana
na wafuasi wao walimvamia na kumfanyia vurugu
zilizosababisha uharibifu wa miwani yake ya macho, vifaa, nyaraka na upotevu wa
baadhi ya vitu.
Alisema kufuatia fujo hizo alifika katika kituo cha Polisi Kisutu nao
wakamueleza hawana mamlaka ya kushughulikia kesi za kisiasa hivyo alifikishe
suala hilo kituo kikuu cha kati cha Polisi.
Hassanali alisema baada yakushauliwa hivyo, aliamua
kwenda kituo hicho lakini cha kusikitisha hakuweza kupata ushirikiano wa
kutosha na alitakiwa kurudi kituoni hapo siku ya Jumatatu (jana), ambapo
alifanya hivyo.
“Leo kama mnavyoniona hapa bado nasumbuliwa nataka
kufungua jalada lakini bado wahusika wanazunguuka tu kwa kunieleza kuwa
msimamizi wa shauri langu hajafika hata hivyo niliweza kuhojiwa na kuandika
maelezo yangu,”alisema.
Wakili wa Hasanali Fredrick Kihwelo, alikiri mteaja wake
kufanyiwa vurugu na kwamba baada ya kufika polisi waliandika maelezo na
kuambiwa uchunguzi unaendelea.
“Pamoja na
kukwama siku ya Jumamosi, leo (jana), tumekuja tena, tangu asubuhi tuko hapa na
hatimaye tumefungua kesi ya jinai kimsingi suala hili litakuwa kwenye uchunguzi
baada ya hapo litapelekwa kwa DPP ambaye ndio ataamua kama litapelekwa
mahakamani.
Kwa upande wake katibu Kata ya wa CCM kata ya Kisutu Sauda, alisema
zoezi la kubandika picha za wagombea limefanyika jiji zima kisheria tangu miaka
ya nyuma na hakutegemea katika eneo hilo kama angekuwepo mtanzania mwenye asili
ya Asia asiwe mfuasi wa CCM.
“Sisi hatukujua
kama pale kuna mtu wa Chadema tena Muhindi kama tungejua tusingebandika kwani
kwa zaidi ya mika 25 tumekuwa tukibandika,”alisema.Sauda.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa Ilala Mery Nzuki alisema suala hilo bado liko kwa mkuu wa kituo
kwa ajili ya uchunguzi na mara litakapokamilika litafikishwa kwake kwa hatua
zaidi.




No comments:
Post a Comment