HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

April 18, 2026

KINYANG’ANYIRO CHA ISIMANI CHAPATA JOTO, KISWAGA AJITOSA UBUNGENI

NA DENIS MLOWE, IRINGA 


KINYANG’ANYIRO cha kuwania ubunge wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa kimeanza kushika kasi baada ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga, kujitosa rasmi katika mbio hizo kwa kuchukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hatua hiyo imefanyika katika ofisi za CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni. 

Kwa mujibu wa vyanzo vya chama, idadi ya wagombea 18 wamejiitokeza kuwania nafasi hiyo, jambo linaloashiria ushindani mkali katika kinyang’anyiro hicho cha kupeperusha bendera ya CCM.

Kiswaga anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi waliobobea katika masuala ya utawala, akiwa amewahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali serikalini. Uzoefu huo unatajwa kumpa nafasi ya kuwania kwa ushindani zaidi katika mchakato huo wa ndani wa chama.

Nafasi hiyo ya ubunge imekuwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi, aliyefariki dunia hivi karibuni. Marehemu Lukuvi aliwahi pia kushika wadhifa wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Ajira na Watu Wenye Ulemavu).

Chama hicho kinatarajiwa kukamilisha mchakato wa ndani wa uteuzi wa mgombea wake kabla ya kutangazwa rasmi kwa ratiba ya uchaguzi mdogo na mamlaka husika.

No comments:

Post a Comment

Pages