Dar es Salaam: Benki ya CRDB imetangaza washindi wa droo ya kwanza ya fainali ya kampeni yake ya “Fainali Ndo Mpango na TemboCard Visa”, inayolenga kuhamasisha matumizi ya malipo yasiyotumia fedha taslimu nchini.
Washindi hao walipatikana katika droo iliyochezeshwa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuhamasisha matumizi ya kadi katika miamala ya kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya benki hiyo, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Kadi, Karington Chahe, amesema kampeni hiyo inalenga kubadili mtazamo wa matumizi ya fedha kwa kuhimiza matumizi ya kadi badala ya fedha taslimu, huku wateja wakipata nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali.
Katika droo hiyo ya kwanza, jumla ya washindi saba walipatikana, ambapo wanne walijishindia safari ya kwenda Marekani kushuhudia fainali za Kombe la Dunia 2026, huku wengine watatu wakijishindia runinga janja (Smart TV) za inchi 85 zenye king’amuzi kilicholipiwa.
Washindi wa safari ya Marekani ni Kenneth Masana Bina (Kagera), Gasper Melkiory Kavishe (Morogoro), Arnold John Samugabo (Dar es Salaam) na Erick Harison Mlinga (Dar es Salaam).
Kwa upande wa washindi wa runinga ni Samson Charles Mkumbo (Dar es Salaam), Theresia Kennedy Mawalla (Dar es Salaam) pamoja na Eunice Aloyce Masigati (Dodoma).
Chahe amesema kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi Machi 12, 2026, ikiwa na lengo la kuwapa Watanzania fursa ya kipekee ya kushuhudia moja ya mashindano makubwa ya soka duniani yatakayofanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
Ameongeza kuwa jumla ya washindi 20 wanatarajiwa kupatikana ifikapo mwisho wa kampeni hiyo mwezi Juni mwaka huu, ambapo 10 watapata nafasi ya kusafiri kwenda kushuhudia Kombe la Dunia, huku wengine 10 wakijishindia runinga janja.
Kampeni hiyo pia inasindikizwa na balozi wake, DJ Ally B, anayehamasisha matumizi ya kadi kwa njia ya kisasa.
Benki ya CRDB imewataka wateja wake kuendelea kutumia TemboCard Visa katika miamala yao ya kila siku ili kuongeza nafasi ya kushinda, huku droo nyingine zikitarajiwa kuendelea kufanyika hadi mwisho wa kampeni hiyo mwezi Juni.




No comments:
Post a Comment