Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu kunyongwa hadi kufa washitakiwa sita
katika kesi ya mauji ya polisi na mafanyakazi wa NMB
tawi la Wami Morogoro na kuiba kiasi cha shilingi milioni 150.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Jaji Projest Rugazia ambaye alianza kuisoma kuanzia saa 10:02 asubuhi
hadi saa 12:20 mchana, huku akitumia lugha ya Kiswahili kusoma hukumu hiyo kwa taratibu
ili kila mtu aelewe.
Washtakiwa hao ambao wamehukumiwa kunyongwa
hadi kufa ni Mashaka Pastory, John Mndasha, Martine Mndasha, Haji Kiweru,
Wycliff Imbora na Rashidi Abdikadir, huku wengine nane wakiachiwa huru.
Jaji Rugazia alisema aliwatia hatiani
washtakiwa hao na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa, kufuatia ushahidi
ulitolewa na mashahidi 29 wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo 78
vilivyowasilishwa mahakamani hapo na ushahidi wa utetezi.
“Maungamo ya washtakiwa, ushahidi wa
kitaalam na utambuzi wa washtakiwa kutambuliwa eneo la tukio inaonesha wazi
walikuwa na nia ya kujaribu kupora Sh 150 milioni mali ya benki ya NMB
zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro tawi
la Wami.” Alisema Jaji Rugazia.
Jaji Rugazia alieleza kwamba, katika
siku hiyo ya huzuni Aprili 20, 2006 mashitakiwa hao walilivamia
gari kwa lengo la kupora lakini bila ya kuwa na huruma yoyote
walilimiminia risasi na kuwaua D 6866 Konstebo Abdallah Marwa na
mfanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro, Ernest Manyonyi.
Akizidi kufafanua kwa hali ya ustadi na
utaratibu, Jaji huyo alisema tukio hilo la kusikitisha lilifanyika nyakati za
saa 6:30 mchana, eneo la Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam kwenye makutano ya
barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Jaji
Rugazia alisema miongoni mwa kundi hilo la majambazi ambao walikuwa 14 kuna
baadhi yao wameokoka na adhabu ya kunyongwa hadi kifo baada ya kuona hawana
hatia.
Aliwataja watu hao, huku baadhi ya
ndugu na jamaa waliokuwa ndani ya mahakama wakibubujikwa na machozi kuwa ni Rashid
Lemblisi, Philipo Mushi, Yassin Juma,Hamisi Daud.
Wengine ni MT 77754 Nazareth Amurike, MT 76162 Emmanuel Lameck, James Chamangwana na Hussein Idd baada ya kuwaona hawana
hatia katika kesi hiyo.
Kwa upande wa washtakiwa, Jackson
Issawangu aliyekuwa mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo na Mussa Mustafa
aliyekuwa mshtakiwa wa 10 waliachiwa huru awali baada ya mahakama hiyo kuwaona
kuwa hawana kesi ya kujibu.
Hadi wanaachiwa huru jana,
washtakiwa hao walikuwa wamekwisha kaa rumande kwa muda wa zaidi ya miaka 8.
Awali, wakati wa usikilizwaji wa kesi
hiyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali vielelezo muhimu vya ushahidi katika kesi
hiyo ya mauaji ikiwemo ripoti saba, kati ya nane za uchunguzi wa silaha
zilizotumika katika mauaji hayo.
Baada ya Mrakibu Msaidizi wa Polisi
(ASP) Godfrey Luhamba, Mtaalam wa milipuko kuiomba mahakama hiyo ipokee
ripoti hizo kama vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo.
Mawakili wa upande wa utetezi
wakiongozwa na Richard Rweyongeza, walipinga ripoti hizo kupokewa, wakidai kuwa
ziliwasilishwa kinyume cha sheria kwa kuwa hazikusomwa kwa washtakiwa wakati wa
kuhamisha kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu.
Katika uamuzi wake, Jaji
Rugazia alikubaliana na utetezi kuwa kwa kuwa ripoti hizo hazikuwahi
kusomwa kwa washtakiwa, basi mahakama hiyo haiwezi kuzipokea kwa kuwa
uwasilishwaji wake ulikuwa ni kinyume sheria.
Pia alikataa hoja za upande wa mashtaka
kutaka mahakama iamuru washtakiwa hao warudishwe tena mahakama ya chini
(Kisutu), wakasomewe ripoti hizo, au iamuru upande wa mashtaka uwapatia upande
wa utetezi wapate muda wa kuzipitia na kisha kuendelea.
Alisema kuwa mapendekezo hayo ya upande
wa mashtaka hayaungwi mkono na kifungu chochote cha sheria.
Hata hivyo mahakama hiyo ilipokea
ripoti moja tu ambayo ndio iliyosomwa kwa washtakiwa katika mahakama ya chini,
ambayo inabainisha kuwa maganda mawili ya risasi, yaliyopatikana katika eneo ya
tukio yalitoka kwenye bastola mojawapo, zilizokamatwa kwa washtakiwa.
Ripoti nyingine zilizokataliwa zinahusu
bastola nane, na SMG 5 na Shortgun moja, ambazo zote zilikamatwa kwa
washtakiwa.
No comments:
Post a Comment