HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 01, 2015

Benki ya CRDB na kampuni ya Bima ya Heritage zanyakua tuzo za BBLA 2014

 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Charles Kitwanga, (Kushoto) akimkabidhi tuzo mshindi wa Tuzo za Bodi yenye Uongozi Bora za 2014 (BBLA) katika sekta ya kibenki, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB Bw. Martin Mmari (kulia). Benki ya CRDB iliibuka mshindi katika sekta ya kibenki wakati kampuni ya Heritage Insurance iliibuka kinara katika sekta ya bima katika tuzo hizo zilizofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. (Picha Mpiga Picha Wetu)
 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Charles Kitwanga, (Kushoto) akimkabidhi tuzo mshindi wa Tuzo za Bodi yenye Uongozi Bora za 2014 (BBLA) katika sekta ya bima, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni ya Heritage Insurance, Bw. Yogesh Manek (kulia). Heritage Insurance iliibuka mshindi katika sekta ya bima wakati Benki ya CRDB iliibuka kinara katika sekta ya kibenki katika tuzo hizo zilizofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Wetu

Benki ya CRDB pamoja na kampuni ya Bima ya Heritage mwishoni mwa wiki zilifanikiwa kuibuka washindi wa tuzo za bodi bora katika sekta ya fedha kwa mwaka 2014 tukio lililofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Benki ya CRDB ilifanikiwa kutwaa tuzo hiyo dhidi ya benki ya Exim iliyofanikiwa kuwa mshindi wa pili huku benki ya Posta (TPB) nayo ikiibuka mshindi wa tatu katika tuzo hizo zilizofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.

Kwa upande wa makampuni ya Bima, Kampuni ya Bima ya Alliance Insurance Corporation ilifanikiwa kutwaa tuzo hiyo baada ya kuibuka mshindi wa kwanza huku ikifuatiwa na kampuni za Alliance Insurance Corporation, Alliance Life Assurance pamoja na Strategies Insurance (T) Limited kwa mtiririko mahususi.

Akizungumzia mchakato mzima wa kupatikana kwa washindi hao, Mwenyekiti wa timu ya majaji wa tuzo hizo Bw. Leonard Mususa alisema, jopo lake liliundwa na watu wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya uongozi katika sekta za fedha akiwamo Mkaguzi mkuu na mdhibiti wa hesabu za serikali (CAG) aliyestaafu, Bw Ludovick Utouh.

Wengine ni pamoja na Bw. Mwaremi Marwa, (Mkurugenzi Mkuu wa soko la Hisa la Dar es Salaam( DSE), Bw. Yona Killaghane (Mkurugenzi mkuu mstaafu wa shirika la maendeleo la Petroli nchini (TPDC).

Aidha akizungumza kwenye hafla hiyo Mwenyeki wa taasisi ya sekta binafsi (TPSF), na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dr Reginald Mengi alisema tuzo zimekuja wakati muafaka kwa kuwa sekta za fedha na Bima nchini zinapitia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, mratibu wa tuzo hizo Bi Neema Gelard alisema tuzo hizo zitatoa mwanga zaidi kuhusuana na namna jinsi bodi bora katika sekta za fedha na bima hapa nchini zinatakiwa kujiendesha.

Zaidi Bi Neema aliwashukuru wadhamini wa tuzo hizo ambao ni kampuni za Capital Plus International (CPI), IPP Media, Real PR Solutions Limited, Afrimax Strategic Partnerships Limited, Serena Hotel, Fix Agency Ltd, Lilacnshades na Excel Management and Outsourcing.

Aidha akizungumza kwenye hafla hiyo naibu waziri wa nishati na makini Bw Charles Kitwanga alitoa wito kwa taaisisi nyingine za fedha na mashirika ya bima kujitokeza na kushiriki katika tuzo zijazo.

''Wakati nawashukuru waandaaji wa tuzo hizi kwa kuja na wazo hili lenye tija kubwa kwa taifa... Naomba nitoe wito kwa bodi za mifuko yetu ya jamii pia ziangalie uwezekano wa kushiriki kwenye tuzo hizi kwa manufaa ya wanachama wa mifuko hiyo''alisema Mhe. Kitwanga.

No comments:

Post a Comment

Pages