HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 21, 2015

FAINALI DARAJA LA KWANZA KUCHEZWA CHAMAZI

Fainali ya kumsaka Bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), inatarajiwa kufanyika kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi kuanzia majira ya saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Awali mchezo huo wa fainali ulikuwa umepangwa kufanyika jumapili kwenye dimba la Uwanja wa Taifa, lakini kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TTF imepelekea mchezo huo kuhamishiwa Chamazi.

Mchezo huo wa fainali utazikutanisha timu za Mwadui ya shinyanga na Toto African ya Mwanza utaanza saa 10 kamili jioni, na utaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha Azam TV ili kuwapa nafasi wapenzi na wadau wa soka waliopo mbali na hasa mikoani kuweza kushuhudia mchezo huo.

Bingwa wa Fainali ya Ligi Daraja la Kwanza atazawadiwa Kombe pamoja na medali, huku mshindi wa pili akipata kikombe na medali pia.

Viingilio vya mchezo huo ni tsh.5,000 kwa jukwaa kuu na tsh. 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko.

Wakati huo huo, Ligi Kuu ya Vodacom inaendelea leo (Jumamosi)  katika viwanja vitatu tofauti, Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Ndanda FC ya Mtwara watawakaribisha Wagosi wa Kaya timu ya Coastal Union kutoka jijini Tanga katika mchezo utakaochezwa kwenye dimba la Ngwanda Sijaona.

Huku wakata miwa wa Kagera Sugar wanaoutimia Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakiwakaribisha Maafande wa Jeshi la Polisi kutoka mjini Morogoro timu ya Polisi.

Ligi hiyo ya Vodacom itaendelea tena kesho jumapili katika viwanja vitatu   tofauti, Uwanja wa Chamazi wenyeji Azam FC wataikaribisha timu ya maafande wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania Prisons, mchezo utakaonza majira ya saa 2 kamili usiku.

Mjini Shinyanga wenyeji timu ya Stand United wataikaribisha Simba SC kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku wagonga nyundo wa jiji la Mbeya, timu ya Mbeya City wakicheza na timu ya Young Africans kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages