MKURUGENZI wa Kampuni ya
Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama akikabidhi misaada kwa mmoja
wa viongozi wa vituo vitano vya kulea yatima ikiwa ni utaratibu wa kusaidia
makundi maalumu. Msaada huo uliotolewa jana katika Ofisi za Gazeti la Dira
Mtanzania, Kinondoni, ni sehemu ya mapato ya Tamasha la Pasaka la mwaka
2014. (Picha na Loveness Bernard)
MWENYEKITI
wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, Alex Msama, ameelezea kuguswa
kwake na wimbi la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi akisema kuwa ni ukatili
uliopitiliza, ambao hata wanyama wa jamii moja hawawezi kufanyiana huku akitoa wito
kwa serikali kuongeza kasi ya kupambana na laana hiyo inayolinyemelea taifa.
Msama
alisema haiingii akilini kuona watu wakifanya ukatili wa kiwango cha kutisha
eti kwa imani kuwa wakifanya hivyo wanaweza kupata mafanikio ya utajiri katika
maisha yao bila kutambua kuwa huko ni kutafuta laana ya Mungu kwa sababu
vitendo hivyo si tu havipendezi mbele ya Mungu, bali hata machoni pa wanadamu.
Msama
ambaye ni miongoni mwa wadau wa kuhimiza amani na upendo katika jamii ikiwa ni
moja ya malengo ya matamasha ya Injili ambayo amekuwa akiyaratibu tangu mwaka
2000, aliyasema hayo jana wakati akitoa misaada ya kiutu kwa vituo vitano vya
kulea yatima vya jijini Dar es Salaam kuelekea Tamasha la Pasaka la mwaka huu.
Katika
hafla hiyo iliyofanyika ofisini kwake eneo la Kinondoni na kuhudhuriwa na
watoto na viongozi wa vituo hivyo pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya
kijamii, Msama alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa jamii kuyasaidia makundi
maalumu kama watoto yatima na walemavu kwa ujumla wake wakiwamo albino waliopo
katika hatari kubwa.
Msama
ametoa wito kwa serikali kuongeza kazi na mbinu mpya za kupambana na watu
wanaojihusisha na vitendo hivyo ambavyo si tu ni ukatili uliopitiliza na
ukiukwaji wa haki za binadamu na mafundisho ya Neno la Mungu, pia ni vitendo vinavyolipaka
matope taifa katika uso wa kimataifa.
Alikwenda
mbali na kushauri serikali kuona umuhimu wa kubuni njia bora ya kuwanusuru
watoto wenye ulemavu huo kwa namna yoyote, ikiwezekana kijengwe kituo maalumu
cha kuwatunza, pia hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika wa mauaji
hayo ambayo yanakwenda kinyume cha haki ya mtu kuishi na kuthaminiwa utu wake.
Msama
amesema kwa usikivu wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, anamsihi kabla ya kumaliza
kipindi chake baadaye mwaka huu angeliangalia upya suala hilo kwa lengo la kuepusha
uhai wa jamii hiyo inayoishi kwa hofu kubwa juu ya usalama wao.
“Najua
Rais wetu mpendwa (Jakaya Kikwete) ni msikivu na mwenye huruma na makundi haya
maalumu katika jamii,
sisi
waratibu wa Tamasha la Pasaka tungemsihi suala hili la mauaji ya albino litafutiwe
dawa huku watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino) wakijengewa makazi yao maalumu,”
alisema.
Alisema
kwa vile suala la amani na upendo ni moja ya ajenda ambazo zimekuwa zikihimizwa
kupitia Tamasha la Pasaka, wataendelea kuhimiza vita dhidi ya vitendo hivyo vibaya
si tu mbele za Mungu, bali hata machoni mwa wanadamu, ili Tanzania iendelee
kuwa sehemu salama ya kuishi.
Mapema
mwezi huu, mwili wa mtoto albino, Yohana Bahati (mwaka mmoja) aliyekuwa
ameporwa kutoka mikononi mwa mama yake katika Kijiji cha Lumasa, Wilaya ya
Geita, Mkoa wa Geita, ulipatikana katika pori la Hifadhi ya Biharamulo,
lililoko Wilaya ya Biharamulo, Mkoa wa Kagera, ukiwa umenyofolewa mikono na
miguu.
Kuhusu
misada, Msama jana alikabidhi misaada ya vitu mbalimbali vikiwamo unga, mafuta
ya kupikia, mafuta ya kupaka, sabuni na sukari kwa vikundi hivyo vitano,
misaada yote ikiwa na thamani ya shilingi mil. 5; ikiwa ni kutambua wajibu wa jamii
nzima katika kuyasaidia makundi maalumu.
Vituo
vilivyopata msaada huo ni Malaika Kids,
Honoratha, Maunga Centre, Mwandaliwa na Istikama, vyote vya jijini Dar es
Salaam, ambapo baada ya kukabidhi, Msama alitoa wito kwa wengine wenye uwezo na
jamii kwa ujumla kujenga utamaduni wa kusaidia wenye mahitaji maalumu.
Msama
Promotions wametoa msaada huo wakiwa katika maandalizi ya Tamasha la Pasaka
litakaloanzia jijini Dar es Salaam, Aprili 5 kabla ya kusambaa katika mikoa
mbalimbali likibeba malengo mbalimbali, ikiwemo shangwe za miaka
15
tangu lianzishwe.
No comments:
Post a Comment