Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Mhe. Mhandisi Christopher Chiza aliwaeleza baadhi ya
wafanyabiashara kutoka Tanzania, kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji
visiwani humo wakati alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro akiwa na
baadhi ya wafanyabiashara Ijumaa tarehe 24 Aprili, 2015 kuonana na Balozi wa
Tanzania Visiwani Comoro Bw. Chabaka Kilumanga na kupata maelezo juu ya kazi
zinazofanywa na Ubalozi huo Visiwani humo.
Akizungumza na
wafanyabiashara Ubalozini hapo Waziri Chiza aliwaeleza kuwa, zipo fursa nyingi
ambazo wanaweza kuzitumia kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania katika visiwa
hivyo na kuangalia namna ya kutumia nafasi hiyo.
“Zipo nafasi nyingi za
kibiashara na uwekezaji, kinachotupasa watanzania ni kuwa na nia ya dhati na
mwamko wa kwenda kuangalia nafasi za biashara kwa nchi za wenzetu japo zipo
changamoto kama za usafirishaji wa bidhaa kwenda visiwani Comoro lakini
tukijipanga vema tutaweza kuzikabili changamoto hizo ambapo tutaweza kujenga
mahusiano makubwa na mazuri ya kibiashara kati kati ya nchi hizi mbili”
alisisitiza Mhe. Chiza.
Akizungumza na
wafabyabiashara hao, balozi wa Tanzania Visiwani Comoro Bw. Chabaka Kilumanga alieleza
kuwa, Ubalozi wake umejipanga kutangaza nafasi za uwekezaji na shughuli ambazo
Tanzania inaweza kuzifanya nchini Comoro ili kuweza kupanua wigo wa uwekezaji
na kujitangaza zaidi Visiwani humo.
“ipo haja ya kufanya
maonesho ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi kama hatua moja wapo ya kukuza soko
la bidhaa za Tanzania na hii itasaidia kuonesha ni nini Tanzania na Comoro
inaweza kufanya kwa pamoja ili kuweza kukuza uchumi kwa nchi hizi
mbili”,alisema.
Bw. Chilumanga alieleza
kuwa, Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro unategemea kuanzisha Tume ya Pamoja
ya ushirikiano kati ya Tanzania na Comoro utakaosaidia kurahisha masuala ya
Uwekezaji na Biashara, na shughuli zingine za kibalozi visiwani humo.
Imetolewa na Francisca Swai
Afisa Habari, Kitengo cha
Mawasiliano
Ofisi ya Waziri Mkuu -
Comoro
27 Aprili, 2015
No comments:
Post a Comment