Na Mwandishi Wetu, Mvomero
BAADA ya wananchi, viongozi wa siasa,
serikali, dini na polisi mkoani Morogoro kushusha pumzi ya kuona matukio ya wizi
sugu wa jambazi la kutisha, Frank Mwambaswa, maarufu kama Geuka, hata familia yake
haikumuingiza nyumbani ili aagwe wala kumuwekea matanga.
Mwambalaswa aliuawa kwa kuchomwa mishale
miwili majira ya usiku hivi karibuni kijijini kwake (Kunke), Kata ya Mtibwa,
Wilaya ya Mvomero, pale alipovunja na kuingia kuiba dukani kwa Stephen Sanga,
ambaye amekuwa akimwibia kila mara na kuahidi kuwaua yeye na mkewe.
Sababu za kuwaibia na kutaka kuwaua
zilibainika kwenye msiba huo kuwa ni kutokana na wao kumkodisha mashine ya
kukatia mbao (chain saw), ambapo kila walipomuulizia kuhusu malipo hata kupitia
kwa ndugu zake, alitoa vitisho hivyo kwa ndugu zake, ambao waliogopa kumwambia mdai.
Siku ya tukio, Mwambalaswa ambaye mwaka
1993 alifungwa miaka 15 jela kwa makosa kama hayo na uuaji, alivunja nyumba ya
Sanga na kuingia ndani, ambapo alibeba vitu vya kwanza ikiwemo jenereta na
kuviweka nje, na aliporudia vingine ili hatimaye awaue Sanga na mkewe, walinzi
walimpiga mishale miwili.
Mwambalaswa alijitahidi kukimbia na
mishale hiyo, lakini sumu yake ilimfanya akate roho kwenye uwanja wa Shule ya
Msingi Kunke, ambapo alifuatwa na kuburuzwa hadi kwenye vitu alivyoiba.
Jeshi la Polisi kwa upande wake,
baada ya kupewa taarifa hizo na kuthibitisha wizi uliofanywa, lilifanya
taratibu zinazostahili na kuamuru familia imzike marehemu, ambapo familia
haikutaka hata aingizwe ndani, bali waliamuru azikwe na kutangaza kuwa
hakutakuwa na matanga.
Aidha, wananchi, viongozi wa vyama
vya siasa, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kutetea haki za binadamu,
yalikuwa na kigugumizi kutetea suala hilo, badala yake
walilaani tabia ya marehemu, ambaye kimsingi aliogopwa.
Watu mbalimbali walioibiwa na
kufanyiwa unyama na jambazi huyo walikuwa wakishangilia, huku wakiionya jamii
kuwa malipo ya matendo mabaya yapo hapa hapa duniani.
No comments:
Post a Comment