HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 18, 2015

TANZANIA KUTUPA KARATA YAKE YA KWANZA LEO KATIKA MICHUANO YA COSAFA

 Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' wakiwa katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao wa Kombe la COSAFA dhidi ya Swaziland utakaochezwa kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng nchini Afrika Kusini.
 
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
 
TIMU ya Taifa ya Soka Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kuanza kutupa karata yake ya kwanza katika michuano ya Kombe la Cosafa dhidi ya Swaziland kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng nchini Afrika Kusini.

Stars, inashiriki michuano hiyo ikiwa nchi alikwa pamoja na Ghana, ambako awali mchezo huo wa Kundi B, ulikuwa ufanyike Uwanja wa Olympia Park, lakini waandaaji wa michuano kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao, imeshindikana kufanyika katika uwanja huo.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, aliyeko nchini humo, Uwanja wa Royal Bafokeng ni miongoni mwa viwanja vilivyotumika katika Fainali za Kombe la Dunia 2010, ukiwa na uwezo wa kubeba watazamaji 42,000 huku timu ya Platinum Stars iliyopo Ligi Kuu ikiutumia kama uwanja wake wa nyumbani.

Kizuguto, alisema wana imani kubwa Stars itafanya vyema katika mchezo huo, kutokana na maandalizi waliyoyafanya, ambako wamekuwa wakijifua kwenye Uwanja wa Shule ya Rustenburg chini ya Kocha Mkuu Mart Nooij na wachezaji wote wako katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo wa leo.

Aliongeza kuwa, jana jioni Stars ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng kwa ajili ya kuuzoea kabla ya mchezo dhidi ya Swaziland leo.

Aidha, Kizuguto aliongeza kuwa, wachezaji wameizoea hali ya hewa, japokuwa kuna baridi lakini hakuna mchezaji aliyeshindwa kufanya mazoezi kutokana na hali hiyo huku akiwaomba Watanzania kuiombea dua.

Baada ya mchezo wa leo, Stars itashuka dimbani tena Mei 20 dhidi ya Madagascar na kuhitimisha makundi hapo Mei 22 na Lesotho. Mshindi wa kundi B atacheza robo fainali dhidi ya timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’.
 CHANZO TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment

Pages