HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 23, 2015

MAMBA WANAOUA WATU KUDHIBITIWA-MASASI

 Katibu Tawala wilaya ya Masasi, Dunford Peter akimwonyesha ramani Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ya sehemu ya mto huo, wakati waziri huyo alipotembelea mto Ruvuma katika kijiji cha Manyuli ambako alitembelea.
 Diwani wa Nhavila, wilayani Masasi Meja Ramadhan Chilumba akimwongoza Waziri wa maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alipotembelea mto Ruvuma katika kijiji cha Manyuli wilayani Masasi, mpakani na Msumbiji alikokwenda kutoa kifutajasho kwa watu waliojeruhiwa na kuuawa na mamba katika mto huo.
Wanakijiji wa Manyuli, wilayani Masasi wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alipozungumza nao jana, alitembelea watu waliojeruhiwa na wengine kuuawa na mamba, alipokwenda kutoa kifuta machozi kutoka wizarani kwake.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amewaagiza askari na maofisa wa wanyamapori nchini kuwavuna mamba wanaoua na kujeruhi wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Manyuli wilayani Masasi mkoani Mtwara, alipokwenda kukagua madhara yatokanayo na mamba katika Mto Ruvuma.
Kauli ya Nyalandu imetokana na kilio cha Mbunge wa Masasi, Mariam Masembe na wananchi wake kuwa mamba hao mbali na kuua na kujeruhi wananchi, pia wamekuwa kero kubwa na kusababisha shughuli za uzalishaji mali kuzorota.

Amesema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imesikia kilio cha wananchi na imeanza kuchukua hatua ili kuhakikisha usalama wa wananchi unakuwepo muda wote na kwamba, jukumu la kuwavuna wanyama hao litasimamiwa na maofisa na askari wa wanyamapori.

“Nimekuja hapa kuwajulia hali na kuwapa pole kutokana na uharibifu wa wanyama hawa ambao wamekuwa wakiwasumbua kwa muda mrefu… nimewaona na kuzungumza na watu waliojeruhiwa na mamba wakati wakiwa kwenye shughuli za uzalishaji mali jirani na mto.

“Watendaji na askari wa wanyamapori kukagua maeneo yote ambayo yana wanyama wanaoshambulia wananchi na kuwajeruhi ili wavunwe. Serikali ya CCM ipo kwa ajili ya maendeleo na kulinda maisha ya watu wake hivyo, wanyama hawa watavunwa haraka iwezekanavyo,” alisema Nyalandu.

Nyalandu amesema kuwa mapato yatakayopatikana kwa kuvunwa mamba hao zitatumika katika mapambano dhidi ya ujangili na huduma zingine za kijamii.

Awali, alikabidhi hundi ya sh. milioni 11.7 ikiwa ni malipo ya kifuta jasho na pole kwa watu walioshambuliwa na mamba wilayani humo, ambapo uongozi wa wilaya utakuwa na jukumu la kugawa kwa utaratibu uliopangwa.

“Kwa kutambua na kuthamini wananchi wetu, serikali yenu ya CCM imetoa fedha kama pole na kifuta jasho kwa ndugu zetu walioshambuliwa na wanyama hawa…fedha hizi haziwezi kuponya machungu ama kurejesha kiungo kilichopotea, lakini ni ubinadamu na kuonyesha kuguswa kwetu na matukio haya,” aliongeza.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Masasi, Dunford Peter, alimpongeza Nyalandu kwa kutimiza ahadi ya kukutana na kuzungumza na wananchi na kutoa kifuta jasho kwa waathirika.

Diwani wa Kata ya Mhavila, Meja Ramadhani Chilumba, alisema Nyalandu ni kiongozi wa aina yake na kwamba, utendaji kazi wake umedhihirisha serikali ya CCM inawajali wananchi wake.

Pia alipongeza uamuzi wa serikali kuvuna mamba katika mto huo kuwa itaongeza ari na hamasa ya wananchi kufanya shughuli za uzalishaji mali bila hofu tofauti na ilivyo sasa.

No comments:

Post a Comment

Pages