Kikosi cha Stars kikijifua. |
Msafara
wa timu ya Taifa ya Tanzania (taifa Stars) inayodhaminiwa na kampuni ya
bia ya Kilimanjaro Premium Lager tayari umewasili salama katika eneo la
Borg El Arab jijini Alexandria na kufikia katika hoteli ya Panacea
tayari kwa mchezo wake wa kesho.
Taifa
Stars ambayo ilikuwa kambini nchini Ethiopia kwa takribani wiki moja,
iliondoka jana usiku Addis Ababa na kuwasili uwanja wa ndege wa Cairo
majira ya saa 8 usiku, kisha kuunganisha kwa usafiri wa basi mpaka Borg
El Arab takribani masaa matatu.
Kocha
mkuu wa Taifa Stars Mart Nooij, atakiongoza kikosi chake katika mazoezi
ya mwisho leo saa 1 usiku katika uwanja wa Borg El Arab kwa saa za
Misri, sawa na saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Akiongelea
mchezo wa kesho, Nooij amesema anashukuru kikosi kimefika salama nchini
Misri na kipo katika hali nzuri, vijana wana ari na morali ya hali ya
juu, anaamini kesho timu itfanya vizuri katika mchezo huo dhidi ya
wenyeji Misri.
Nooij
amesema mchezo wa kesho ni muhimu kwake, na kikosi chake kitacheza mpira
wa kasi na pasi za haraka haraka, huku safu ya ushambuliaji
ikihakikisha inatumia vizuri nafasi itakazozipata.
Aidha
kuelekea katika mchezo huo wa kesho, kiungo Amri Kiemba ameungana na
wachezaji wengine waliokuwa kambini Addis Ababa kuchukua nafasi ya
Mrisho Ngasa ambaye alishindwa kuungana na timu kutokana na sababu
zilizopo nje ya uwezo wake.
Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia tayari
amewasili jijini Alexandria kwa ajili ya kuipa sapoti Taifa Stars katika
mchezo huo wa kesho.
Mchezo
kati ya Misri na Tanzania utachezwa kesho saa 2 usiku kwa saa za Afrika
Mashariki na kati katika uwanja wa jeshi la Misri (Borg El Arab) uliopo
takribani kilometa 70 kutoka jijini Alexandria na kilometa 200 kutoka
jiji la Cairo.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment