NA CLEZENCIA TRYPHONE
KOCHA Mkuu wa Klabu ya Simba Dylan Kerr amesema
atahakikisha anaifuatilia michuano ya Kombe la Kagame iliyoanza kutimua vumbi
juzi hasa zikishuka dimbani Yanga, Azam FC na KMKM za Tanzania.
Kerr Mwingereza aliyetua Simba akichukua mikoba ya Goran
Kopunovic aliyasema hayo juzi katika mchezo wa ufunguzi kati ya Yanga na Gor
Mahia uliopigwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na Yanga kulala kwa mabao
2-1.
Alisema, kutokana na ushindani wa Soka la Tanzania hasa
katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC na Yanga ndio washindani wake wakubwa,
hivyo anatumia nafasi hii kuwasoma kabla ya Ligi kuanza mwishoni mwa mwezi
ujao.
“Nimekuja leo kuwaangalia Yanga, na kesho pia nitakuja
kuwaangalia Azam FC, hiyo inanipa nafasi mimi mwalimu ya kujua aina na jinsi
ambavyo timu hizo zinacheza kabla ya kukutana nazo,”alisema.
Aidha Kerr alisema, Yanga sio timu mbaya ila tatizo lao
linaonekana liko katika safu ya ushambuliaji kwani imeonekana kukosa nafasi
nyingi katika mchezo huo na kujikuta wakifungwa, hivyo ni jukumu la mwalimu wao
kulitazama hilo kabla ya mchezo unaofuata.
Kwa upande wa Gor Mahia Mwingereza huyo, alikiri kuvutiwa
na viwango vya nyota wengi wa timu hiyo, hasa safu ya kiungo kutokana na jinsi
ambavyo iliwatengenezea vema washambuliaji mazingira ya kufunga mabao hayo.
No comments:
Post a Comment