Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Fionnuala Gilsenan, akitoa hotuba yake wakati wa maonyesho ya sayansi kwa wanafunzi wa sekondari yanayoandaliwa na shirika la YST ambayo pia Ubalozi wake unadhamini kila mwaka.
Na Daniel
Mbega
UBALOZI wa
Ireland nchini Tanzania, umewapatia scholarship Watanzania 14 ili kusoma kozi
mbalimbali za shahada ya uzamili (masters) na huku wanne kati yao wakienda kusoma
vyuo vya nje ya nchi hasa University College Dublin, Dublin Institute of
Technology na National University of Ireland Maynooth.
Kwa mujibu
wa taarifa kutoka Ubalozi wa Ireland nchini, scholarship hizo zimetolewa na
ubalozi huo kama sehemu ya Mpango wa Mafunzo wa Kila Mwaka (Fellowship Training
Programme), ambapo wataalamu wanne waliobahatika kwenda ng’ambo watakwenda
kusomea kozi za Maendeleo Endelevu (Sustainable Development), Kilimo na Maisha
ya Vijijini (Agriculture and Rural Livelihoods), Rasilimali Watu (Human
Resource Management), na Immunolojia na Afya ya Binadamu (Immunology and Human
Health).
Watanzania
wengine 10 wamedhaminiwa kusomea kozi mbalimbali katika vyuo vikuu vya hapa
nchini.
Taarifa
hiyo inasema, sherehe za kuwapokea wale walihitimu na kuwakabidhi scholarship
wale wanaokwenda kuanza, zitafanyika kesho mchana katika ofisi za Ubalozi zilizoko
Masaki, jijini Dar es Salaam ambapo Balozi wa Ireland nchini, Fionnuala Gilsenan, ndiye atakayetoa scholarship hizo.
Mpango huo
wa Mafunzo wa kila Mwaka, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa kiasi kikubwa
unahusisha Mfuko wa Misaada wa Ireland (Irish Aid) kupitia program ya maendeleo
ya Ubalozi huo nchini Tanzania.
Wanufaika wa
mpango huo wameteuliwa na washirika wa maendeleo wa Ireland nchini Tanzania,
zikiwemo wizara mbalimbali za Serikali, halmashauri za wilaya na mashirika
yasiyo ya kiserikali, ambayo shughuli zao zinawiana na maeneo ya vipaumbele vya
Irish Aid, hususan Kilimo, Afya, Lishe na Utawala.
Aidha,
wanufaika wote ni watendaji wa kati ambao baada ya kuhitimu masomo yao
watarejea kwenye mashirika na taasisi zao kutumia ujuzi walioupata kwa manufaa
ya jamii.
“Kwa wanufaika
watakaokwenda kusoma nchini Ireland, program inatoa fursa nzuri ya kujifunza
katika hadhi ya kimataifa na kunufaika na hazina kubwa ya nyenzo za tafiti
zinazotolewa kwenye Vyuo Vikuu na Taasisi za Teknolojia za Ireland,” imeeleza
taarifa hiyo.
Ikaongeza:
“Inatarajiwa kwamba mafunzo ya wataalamu hawa yatachangia kwa kiasi kikubwa
maendeleo ya Tanzania, na kuendelea kuimarisha ushirika wa kielimu baina ya
Ireland na Tanzania.”
Ireland,
kupitia Mfuko wa Misaada (Irish Aid), imekuwa ikidhamini Mpango huo wa Mafunzo nchini
Tanzania kwa miaka 40 sasa ambapo program hiyo imekuwa msingi wa msaada katika
kuzijengea uwezo nchi zinazoendelea na inaendana na mkakati wa kupunguza
umaskini wa nchi washirika wa Ireland, hasa lengo likiwa kuwapatia wataalamu
elimu ya juu ili waendeleze taasisi zao.
Baadhi ya
taasisi washirika zitakazonufaika na mpango wa mwaka huu ni pamoja na Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Halmashauri
ya Wilaya ya Kigoma, Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, Halmashauri ya Wilaya ya
Kondoa, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Taasisi
ya Chakula na Lishe, Hospitali ya CCBRT, shirika la Sikika, Mpango wa Maendeleo
wa Kinapa (Kinnapa Development Programme), shirika la CARE Tanzania na Taasisi
ya Afya Ifakara (IHI).
No comments:
Post a Comment