HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 18, 2015

UKAWA WATANGAZA MAJIMBO WALIYOGAWANA KATIKA UCHAGUZI MKUU

 Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi,  Nderakindo Kessy (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho, Ilala Dar es Salaam jana, wakati akitangaza majimbo yaliyochini ya vyama vinavyounda Ukawa ambayo vyama hivyo vitasimamisha wagombea wao katika uchaguzi mkuu. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Masudi Makunjunga. 
 Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Shaweji Mketo (wa pili kulia), akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari. Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Masudi Makunjunga, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi,  Nderakindo Kessy na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika.
 Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, akizungumza katika mkutano huo.
 Viongozi wa vyama hivyo wakiwa meza kuu.

Na Mwandishi Wetu


UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umetangaza mgawanyo wa majimbo yake 253 huku majimbo mengi yakienda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Taarifa ya mgawanyo wa majimbo ilitolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Dk. Nderakindo Kessy jana katika ofisi kuu za chama hicho Ilala jijini Dar es Salaam.

Kessy alisema baada ya majadiliano ya muda mrefu kuhusu kuachiana majimbo ya ubunge, vyama vinavyounda Ukawa vimefanikiwa kuachiana majimbo ili kuhakikisha wanakiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), madarakani.

Alisema mgawanyo wa majimbo hautahusiana na mgawanyo wa kata za kugombea udiwani na mwongozo wa kuachiana kata ndiyo utatumika katika kuamua namna ya kugombea kata.

“Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwatangazia Watanzania majimbo ambayo hadi leo (jana), tumekubaliana kuachiana kuwa ni majimbo 253 na majimbo 12 tutawaambia Jumatano au Alhamis kwani kuna mambo hayajakaa vizuri,” alisema.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Mkoa wa Mara majimbo yote wameachiwa Chadema ambayo ni Rorya, Tarime Mjini, Tarime Vijijini, Musoma Vijijini, Butiama, Bunda Mjini, Mwibara, Musoma Mjini na Bunda Vijijini.

Kessy alisema Mkoa wa Simiyu ambao una majimbo saba, majimbo sita wamepewa Chadema ambayo ni Bariadi, Maswa Magharibi, Maswa Mashariki, Kisesa, Meatu, Itilima na Jimbo la Busega atasimama mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF).

“Mkoa wa Shinyanga majimbo yote sita wameachiwa Chadema na sababu ya msingi ni wao kuwa na mizizi ambapo ni majimbo ya Msalala, Kahama Mjini, Kahama Vijijini, Shinyanga Mjini, Kishapu na Ushetu na Mkoa wa Mwanza ni Ukerewe, Magu, Nyamagana, Buchosa, Sengerema, Ilemela, Misungwi yameenda Chadema na Kwimba na Sumve CUF,” alisema.

Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema Mkoa wa Geita majimbo yote yaliachiwa Chadema, ambayo ni Bukombe, Busanda, Nyang’wale, Chato na Mbogwe, Mkoa wa Kagera katika majimbo tisa Chadema imeachiwa majimbo sita ambayo ni Karagwe, Kyerwa, Bukoba Mjini, Muleba Kaskazini, Muleba Kusini na Biharamulo na Nkenge, Ngara yakiachwa kwa NCCR-Mageuzi na Jimbo la Bukoba Vijiji likiachwa kwa CUF.

Mkoa wa Mbeya Jimbo la Lupa, Songwe, Mbeya Mjini, Kyela, Rungwe, Busekolo, Mbozi Mashariki, Momba, Mbeya Vijijini, Vwawa na Tunduma yote yameachiwa Chadema na Jimbo la Ileje NCCR-Mageuzi.      

“Iringa, Jimbo la Ismani, Kalenga, Mufindi Kaskazini, Iringa Mjini, Kilolo, Mufindi Mjini Chadema itasimamisha wagombea na Mufundi Kusini NCCR-Mageuzi, ambapo Mkoa wa Njombe majimbo yote yameachwa Chadema ambayo ni Njombe Kaskazini, Lupembe, Wanging’ombe, Makete, Ludewa na Makambako,” alisema Kessy.

Kessy alisema Mkoa wa Rukwa wamekubaliana kuwaachia Chadema, ambapo ni majimbo ya Nkasi Kusini, Kwela, Nkasi Kaskazini, Sumbawanga Mjini na Kalambo, huku Mkoa wa Tanga CUF wameachiwa majimbo nane ambayo ni Handeni Mjini, Handeni Vijijini, Pangani, Tanga Mjini, Bumbuli, Mlalo, Lushoto na Mkinga. Chadema wameachiwa majimbo manne ambayo ni Kilindi, Muheza, Korogwe Mjini na Korogwe Vijijini. 

Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema Mkoa wa Kilimanjaro majimbo saba imeachiwa Chadema ambayo ni Rombo, Same Magharibi, Same Mashariki, Moshi Vijijini, Moshi Mjini, Hai na Siha ambapo Vunjo NCCR-Mageuzi wameachiwa na Jimbo la Mwanga likibakia hadi Alhamis.

Mkoa wa Arusha alisema Chadema wameachiwa majimbo yote ambayo ni Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi, Arusha Mjini, Longido, Monduli, Karatu na Ngorongoro halikadhalika Mkoa Manyara Jimbo la Simanjiro, Mbulu Vijijini, Hanang, Babati Mjini, Babati Vijijini, Kiteto na Mbulu Mjini.

Aidha, Kessy alisema Mkoa wa Dar es Salaam, Jimbo la Ubungo, Kawe, Ukonga, Ilala na Kibamba Chadema itasimamisha wagombea na Kinondoni, Jimbo la Temeke na Mbagala CUF itasimamisha wagombea huku majimbo ya Segerea na Kigamboni yakibakia kiporo hadi Alhamisi wiki hii.

Alisema Mkoa wa Pwani majimbo ya Bagamoyo, Kisarawe, Mkuranga, Mafia, Rufiji Utete na Rufiji Kibiti majimbo hayo yameachiwa CUF na Majimbo ya Chalinze, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini yakiachiwa Chadema.    

Mkoa wa Morogoro Jimbo la Kilosa na Morogoro Kusini Mashariki CUF watasimamisha wagombea huku majimbo ya Mikumi, Morogoro Kusini, Kilombero, Mlimba, Mvomero, Ulanga Magharibi, Ulanga Mashariki na Morogoro Mjini yatakuwa chini ya Chadema.

“Mkoa wa Dodoma Jimbo la Kondoa Mjini, Kondoa Vijijini, Chemba yameachwa kwa CUF, Jimbo la Kibakwe na Mtera wameachiwa NCCR-Mageuzi na Dodoma Mjini, Kongwa, Bahi na Chilonwa Chadema itasimamisha wagombea.

Kessy alisema Mkoa wa Singida majimbo yote saba yameenda Chadema ambayo ni Iramba Magharibi, Iramba Mashariki, Singida Kaskazini, Singida Mashariki, Singida Magharibi, Manyoni Magharibi na Manyoni Mashariki. 

Kwa Mkoa wa Tabora Jimbo la Bukene, Nzega Vijijini, Igalula, Kaliua Tabora Kaskazini na Tabora Mjini watagombea CUF na Nzega Mjini, Igunga, Urambo, Ulyankulu, Manonga na Sikonge Chadema watasimamisha wagombea.

Alisema Mkoa wa Katavi majimbo yote sita ya Mpanda Mjini, Mpanda Vijijini, Katavi, Nsimbo na Kavuu. Mkoa wa Kigoma Jimbo la Buyungu, Mhambwe, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini, Kigoma Kusini na Manyovu NCCR-Mageuzi itasimamisha wagombea na Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini Chadema itasisimamisha wagombea wa ubunge.

Mkoa wa Ruvuma Jimbo la Tunduru Kaskazini, Namtumbo na Tunduru Kusini Chama cha CUF watasimamisha wagombea na majimbo ya Peramiho, Mbinga Magharibi/Nyasa, Mbinga Mashariki/Mbinga, Songea Mjini na Madaba, na Mbinga Mjini NCCR-Mageuzi itasimamisha mgombea.

“Mtwara Jimbo la Newala Mjini, Newala Vijijini, Tandahimba, Mtwara Vijijini, Nanyamba na Nanyumbu CUF itasimamisha wagombea huku majimbo ya Lulindi, Masasi na Ndanda wakiachiwa Chama cha National League Democratic (NLD),” alisema Kessy.

Kessy alisema Mkoa wa Lindi Ukawa kwa ujumla wao wamekubaliana kuwaachiwa CUF katika majimbo yote ambayo ni Mtama, Kilwa Kaskazini, Kilwa Kusini, Lindi Mjini, Ruangwa, Nachingwea, Liwale na Mchinga.
Mketo

Akizungumzia uamuzi huo, Kaimu Naibu Katibu Mkuu CUF, Shaweji Mketo alisema mgawanyo huo umezingatia mambo makuu matano ambao ni kuhusu mbunge aliyeko tangu waka 2010, nafasi ya chama katika uchaguzi huo wa 2010, nafasi ya udiwani, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na nguvu na mtandao wa chama hadi sasa.

Mketo alisema lengo la Ukawa si kugawana majimbo kama inavyotafsiriwa ila ni kugawana kwa vigezo ili kuhakikisha wanapata ushindi wa jumla na kushinda uchaguzi ujao.

Makujunga

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa NLD, Masudi Makujunga alisema chama chao kipo pamoja kuhakikisha kuwa mabadiliko ya kisiasa, kijamii yanatokea ndani ya nchi wakati huu.

“Lengo si ufahari katika kugawana majimbo, lengo letu ni kuhakikisha kuwa mabadiliko yanapatikana na sisi NLD tupo tayari kushiriki katika mabadiliko hayo kwenye sehemu husika,” alisema.

Mnyika

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema jitihada za Ukawa zipo katika hali nzuri hivyo wao watahakikisha kuwa wanakuwa wamoja hadi kufikia hatima yao ambayo ni kushinda uchaguzi na kuongoza nchi.

Alisema kilichofanyika ndio makubaliono ya viongozi wao hivyo wana Ukawa wote wanapaswa kukubaliana na hali hiyo ili Taifa liweze kusonga mbele kwa maslahi ya wananchi na wapenda mabadiliko.

Aidha, Mnyika aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutoa ufafanuzi kuhusu kuwepo kwa maelekezo ya kuvitaka na wagombea wao kurejesha fomu Agosti 19, mwaka huu huku ikiamini kuwa sheria inataka mchakato huo kukamilika Agosti 21.

Mnyika aliitaka NEC kutoa ufafanuzi kuhusu kuwepo kwa wanajeshi watatu ambao wanahusika na mfumo wa teknolojia ya habari katika tume hiyo jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za tume hiyo.

Mnyika alisema iwapo tume itakuwa kimya itakuwa imethibitisha taarifa hizo ambazo kimsingi zinachochea vurugu na hofu kwa washiriki wa uchaguzi huo.

Ukawa uliasisiwa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014, lengo likiwa kuunganisha nguvu kwa ajili ya kusimamia na kutetea maoni ya wananchi yaliyowasilishwa kupitia rasimu ya pili ya Katiba iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Umoja huo ulihusisha wabunge kutoka vyama mbalimbali vya upinzani na baadhi ya wabunge kutoka kundi lililojulikana kama la 201ambapo baadaye, ulibaki na wabunge na viongozi kutoka vyama vya NLD, NCCR – Mageuzi, CUF na Chadema.

No comments:

Post a Comment

Pages