Mgombea Urais wa
Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi
wa chama hicho katika fukwe za Nungwi baada ya viwanja vya sokoni Nungwi kuwa
vidogo.
Mgombea Urais wa
Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhiwa jahazi
na wazee wa Nungwi kwenye mkutano wa chama hicho uliofanyika katika fukwe za
Nungwi baada ya viwanja vya sokoni Nungwi kuwa vidogo.
Umati wa watu ukimsikiliza Maalim Seif.
Wafuasi wa CUF
walivyojitokeza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika fukwe za Nungwi
Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Na Hassan Hamad, OMKR
Chama Cha Wananchi
CUF, kimelazimika kufanya mkutano wake wa hadhara katika fukwe za Nungwi, baada
ya kiwanja cha Sokoni Nungwi kuonekana kuwa kidogo kutokana na idadi kubwa ya
wanachama waliojitokeza kwenye mkutano huo.
Katika mkutano huo wa
kampeni Jimbo la Nungwi, mgeni rasmi alikuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kwa
tiketi ya Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.
Akizungumza katika
mkutano huo, Maalim Seif amesema hakuna sababu kwa Chama hicho kukosa ushindi
katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 mwezi huu kutokana na kuungwa mkono na
wanachama wengi katika maeneo yote ya Zanzibar.
Ameelezea
kufurahishwa na jinsi wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja walivyohamasika
kukiunga mkono Chama hicho, na kwamba huo ni ushahidi tosha wa kukiweka chama
hicho madarakani.
Amesema iwapo
atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atashughulikia migogoro ya ardhi
inayojitokeza katika Mkoa huo, baada ya maeneo kadhaa ya wananchi kupewa
wawekezaji bila ya utaratibu unaokubalika.
Aidha amerejea kauli
yake ya kuwarejesha Zanzibar Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho wanaoshikiliwa
Tanzania Bara, wiki moja baada ya kuapishwa kuwa Rais na kwamba kesi yao
itasikilizwa katika Mahakama ya Zanzibar.
Amemshauri Rais wa
Zanzibar kuwadhibiti viongozi wa CCM wenye dhamira ya kuleta vurugu nchini, ili
uchaguzi ujao ufanyike katika hali ya amani na usalama.
Nae Naibu Katibu Mkuu
wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Zanzibar Bw. Salum Mwalim, amewataka
mawakala kuwa makini katika kusimamia kura za wagombea wao.
Amesema vyama
vinavyounda Umoja wa UKAWA havitomvumilia wakala atakayefanya uzembe katika
usimamizi wa kura, na kwamba atakayebainika atawajibishwa.
Kabla
ya Mkutano huo Maalim Seif alitembelea na kufungua barza mbali mbali za Chama
hicho ikiwemo barza ya New Singapore
katika kijiji cha Bwereu Kitogani, na kuelezea kufarajika kwake kutokana na
namna vijana walivyojipanga kukipatia chama hicho ushindi katika uchaguzi ujao.
Wazee
wa Nungwi kwa upande wao wamemkabidhi jahazi Maalim Seif, ili aweze kuliongoza hadi kufikia kupatikana kwa mamlaka kamili ya
Zanzibar.


No comments:
Post a Comment