Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya
Kilimanjaro Premium Lager inarejea leo nyumbani kwa shirika la ndege la
Fastjet, ambapo inatarajiwa kuwasili uwanja wa JK Nyerere majira ya saa
12 kamili jioni.
Stars iliyokuwa imeweka kambi nchini Afrika Kusini kwa takribani siku
10, inarejea nyumbani ikiwa imefanya mazoezi vizuri kujiandaa na
kuwakabili Mbweha wa Jangwani Algeria siku ya Jumamosi katika Uwanja wa
Taifa jijini Dar es salaam.
Akiongelea kuhusu kambi kocha wa Stars, Charles Mkwasa amesema
anashukru kwa kambi waliyoipata Afrika Kusini, wachezaji wote wameweza
kufanya mazoezi katika kiwango cha juu, hapakua na majeruhi hivyo ana
imani vijana wake watafanya vizuri siku ya Jumamosi.
Mkwasa amewaomba watanzania na wapenzi wa mpira wa miguu nchini,
kujitokeza kwa wingi uwanjani kuja kuwasapoti katika mchezo dhidi ya
Algeria, uwepo wa watanzania wengi uwanjani kuwashangilia utaongeza
morali zaidi kwa wachezaji watakaokuwa wanapeperusha bendera ya
Tanzania.
Mara baada ya kuwasili jijini Dar es salaam, kikosi cha Mkwasa
kitafanya mazoezi kesho Alhamis jioni katika uwanja wa Taifa, na Ijumaa
yakiwa ni mazoezi ya mwisho kabisa ya mchezo wenyewe unaosubiriwa kwa
hamu.
Wakati huo huo wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu
wamewasili jijini Dar es salaam leo asubuhi , na moja moja kuingia
kambini huku wakiwasubiri wachezaji wenzao wanaowasili leo na kujumuika
pamoja kambini
No comments:
Post a Comment