Dr.
Judith Odunga Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF akisoma taarifa kwa
vyombo vya habari kuhusiana na kuanza kwa siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia.
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU
Katika kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kuanzia
tarehe 25 Novemba mpaka 10 Desemba, WiLDAF, Mashirika ya Haki za Binadamu,
Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kiraia watatoa elimu na kuhamasisha umma
kuchukua hatua kumlinda mtoto ili apate elimu bora na salama. Ulinzi wa mtoto ni
pamoja na kuzuia vitendo vyote vya ukatili
wa kijinsia.
Maadhismisho ya SIku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia mwaka
huu yanalenga zaidi kuzungumzia suala zima la usalama mashuleni, lengo kuu ikiwa kuhamasisha umma
kuhusu ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa vijana na watoto wetu
mashuleni, kwani vitendo vingi vya ukatili wa kijinsa vimekuwa vikiripotiwa.
Utafiti uliyofanywa na Chuo cha Tiba Cha Muhimbili (MUHAS)
kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika,
(WiLDAF) umetambua hatari zinazochangia ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na
wazazi kutowajali watoto na kutoa adhabu kali kwao na hivyo kuwafanya watoto
kuwa na hofu. Wakati mwingine watoto kufanyiwa ukatili bila wao kufahamu. Aidha,
adhabu ya viboko inahusishwa kama moja ya aina za ukatili dhidi ya watoto. Hii
inaathiri maendeleo ya elimu ya watoto katika taifa letu.
Kukosekana kwa usawa kati ya watoto wa kiume na wa kike hunapelekea
kuwajengea hofu watoto wa kike, na wakati
huo kuwajengea watoto wa kiume ujasiri wa kuona kuwa ni sahihi kwao kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aidha, tafiti kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto (VAC) uliofanywa
na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) wa mwaka 2011 ulionesha
kwamba watoto 3 wa kike kati ya 10 na mtoto 1 kati ya watoto 7 wa kiume wenye
umri kati ya miaka 13-24 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kingono. Aidha, asilimia
6 ya watoto wa kike wamelazimishwa kufanya tendo la ngono kabla ya miaka 18.
Pia utafiti huo unaonesha kuwa watoto wa kike wanafanyiwa vitendo vya kingono na wanaume waliowazidi umri wakati watoto wa
kiume wanafanyiwa ukatili na watoto wenye umri sawa.
Tafiti pia imeonesha kuwa vitendo hivyo vinafanywa na watu
wanaowafahamu wakiwemo majirani, wapenzi wao, watu wenye mamlaka (walimu). Ni asilimia 32.2 tu ya watoto wa kike na
asilimia 16.6 ya watoto wa kiume wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na
watu wasiofahamika na watoto. Vitendo hivi hufanyika maeneo ambayo uangalizi wa
watu wazima unahitajika kuwepo kwa mfano mashuleni, njiani, majumbani na wakati
mwingine katika vyombo vya usafiri.
Ni dhahiri kwamba kwa mazingira, mila na utamaduni
ikijumuisha familia za Kitanzania, vimekuwa vikichangia vitendo vya ukatili wa
kijinsia. Vitendo vya ukatili na udhalilishaji vina madhara makubwa ya kiafya kwa
watoto kwani hukatisha uwezo wao wa kielimu, mahudhurio ya shule na hivyo
kupelekea matokeo mabaya ya katika
ufaulu wao wakati wa mitihani.
Aidha, mazingira yasiyo salama kwa watoto wa shule yana madhara
makubwa. Watoto wanapokuwa mashuleni na kufanyiwa ukatili wa kingono wapo
katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya UKIMWI kwa mathlani mara tatu
zaidi ya wale ambao hawajawahi kufanyiwa ukatili.
Tunaamini kwamba kuondolewa kwa vikwazo vinavyo chochea
ukatili wa kijinsia kwa watoto wa shule kutachangia katika kuleta usawa wa
kijinsia kwa watoto wa kiume na wa kike. Pia mazingira mazuri ya shule yatasaidia
mahudhurio mazuri ya watoto mashuleni na kuleta matokeo mazuri katika ufaulu.
Jamii inahaswa kuweka mazingira mazuri ya shule ikiwa ni
pamoja na kuwepo miundombinu kama mabweni, vyoo, madawati, uzio kuzunguka
mashule na vyombo rafiki vya usafiri. Haya yote yatawezekana tu ikiwa kutakuwa
na dhamira ya dhati kwa watunga sera, wazazi, walimu, wanafunzi na jamii kwa
ujumla katika kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto. Kuna haja
ya makusudi kabisakutofumbia macho
masuala ya ukatili kwa ujumla wake ili kujenga jamii imara.
Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia ni tukio la kimataifa la kila mwaka ili kuwa
na nguvu ya pamoja katika kuzuia kuenea
kwa janga hili . Ndani ya siku hizi, kuna siku zingine muhimu za kimataifa ,
mathlani, Novemba 25 ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake,
Novemba 29 ni Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Desemba 1 ni
Siku ya UKIMWI Duniani, Desemba 3 ni Siku ya Kimataifa ya watu wenye Ulemavu,
Desemba 6 ni Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Mauaji ya kikatili ya Montreal
1989, ambapo wanawake 14 waliuawa na mtu aliyekuwa anawachukia wanawake. Tarehe
hizi zilichaguliwa mahususi ili kuhusianisha kwamba ukatili wa kijinsia unaongeza
maambukizi ya UKIMWI na ni Ukiukwaji wa Haki za Binadamu.
Katika kipindi hiki cha Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili
wa Kijinsia , mamia ya asasi za kiraia na wadau mbalimbali Tanzania wataifikia
jamii kwa kauli mbiu inayosema;
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU.
No comments:
Post a Comment