HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 07, 2016

Wadau wataka Tamasha la Pasaka livuke mipaka

Alex Msama
 Dar es Salaam, Tanzania

WADAU na wapenzi wa muziki wa injili nchini, wametoa wito kwa waratibu wa tamasha la Muziki wa Injili la wakati
wa  Pasaka, Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam, kuongeza wigo wa kufanyika katika nchi zote za Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa mmoja wa mashabiki wa Tamasha hilo linalobeba malengo ya kuutukuza ufalme wa Mungu na mengineyo ikiwemo kupata fedha za kusaidia makundi maalumu katika jamii, Anna Shibamla wa Yombo- Machimbo, jijini Dar es Salaam, umefika wakati sasa tukio hilo likawa la nchi za Afrika Mashariki.

“Unajua Tamasha la Pasaka tayari lina sura ya kimataifa kwa sababu limekuwa likiwaleta pamoja waimbaji kutoka nchi mbalimbali, lakini kwa mawazo yangu umefika wakati sasa likawa linafanyika katika nchi za Afrika Mashariki ambazo
ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi,” alisema Anna.

Anna aliyejitambulisha kama mmoja wa wadau wakubwa wa muziki wa injili na matamasha la Msama Promotions, alisema kwamba kama wazo hilo litafanyiwa kazi, kutalifanya tamasha lenyewe kuwa kubwa zaidi na kubeba maana zaidi kwani linaweza kuwa kielelezo cha umoja na nchi za Afrika Mashariki.

“Kwa mtazamo wangu, ni jambo linalowezekana kama waratibu watakuwa wamejipanga kwa mfano Tamasha la Pasaka likafanyika hapa jijini Dar es Salaam, kisha likaenda kutikisa Nairobi (Kenya); Kigali (Rwanda); Kampala (Uganda) na
kule mjini Bujumbura (Burundi),” aliongeza.

Anna alisema kwa uzoefu wa zaidi ya miaka 16 wa Msama Promotions katika kuandaa tamasha hilo kwa ufanisi, anaamini anaweza kulifanya tukio jhilo kuwa la Afrika Mashariki na likawa na mvuto wa aina yake huku likibeba uzito zaidi katika kutangaza ujumbe wa Neno la Mungu, amani na upendo kuanzia kwa watu hadi kwa nchi za ukanda huo.

Wazo hilo limeungwa mkono na Jasmin Jeremiah wa Ilonga Kilosa, Mkoani Morogoro kwa kusema hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa waimbaji wa nchi moja kufahamika katika ncho zote za ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo kuongeza wigo wa kupata soko la huduma yao ya uimbaji.

“Kama Tamasha la Pasaka litakuwa likifanyika katika nchi zaidi ya moja kwa mwaka, itawapa nafasi waimbaji kwa mfano wa Tanzania kujulikana katika nchi hizo kwa mfano Kenya, Rwanda na Burundi, hivyo sio tu kutaimarisha uhusiano kati ya nchi na nchi, pia itakuwa hivyo kwa waimbaji,” alisema Jasmine akiungwa mkono na Neema Gerald.

Neema alisema kitendo cha waimbaji wa nje kama Rebecca Malope wa Afrika Kusini ana Anastazia Mukabwa wa Kenya wakaenda kutumbuiza katika Tamasha la Pasaka nchini Rwanda au Burundi, kutaleta mvuto zaidi wa tukio hilo na kusema  anaunga mkono suala hilo kwa asilimia 100.

Wazo hilo la wadau ni kutokana na tamasha hilo lililoasisiwa tangu mwaka 2000, limekuwa likifanyika nchini kwa kuanzia jijini Dar es Salaam na katika mikoa kadhaa, hivyo maoni ya wadau ni tukio hilo kwenda mbali zaidi ya hapo kwamba liwe linafanyika katika nchi zaidi ya moja katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alipotafutwa kuhusu maoni hayo ya wadau, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizii ya Tamasha hilo, Alex Msama, alisema
ni wazo zuri kwani huduma na malengo yake vitazidi kupanuka na kubeba sura ya kimataifa zaidi ikiwemo kuwa kielelezo cha umoja na mshikamano wa nchi za Afrika Mashariki na kuongeza wataketi kutafakari suala hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages