HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 16, 2016

BALOZI WA PEPSI AJIPANGA KUFANYA KOLABO NA ALLY KIBA, BELLA

Balozi wa kinywaji cha Pepsi ambaye ni msanii kutoka Nigeria, Seyi Shay (katikati), akionyesha umahiri wa kuimba na kucheza mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja Masoko wa SBL, Roselyne Bruno na Mkuu wa Masoko, Catherine Arlen. Msanii huyo alibainisha kuwa anaweza kushirikia na baadhi ya wanamuziki wa Tanzania akiwemo Ally Kiba.   (Picha na Francis Dande)
Balozi wa kinywaji cha Pepsi ambaye ni msanii kutoka Nigeria, Seyi Shay (katikati), akionyesha umahiri wa kuimba na kucheza mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam juzi. Kushoto ni Meneja Masoko wa SBL, Roselyne Bruno na Mkuu wa Masoko, Catherine Arlen.  
 Balozi wa kinywaji cha Pepsi ambaye ni msanii kutoka Nigeria, Seyi Shay (katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja Masoko wa SBL, Roselyne Bruno na Mkuu wa Masoko, Catherine Arlen. 
Balozi wa kinywaji cha Pepsi ambaye ni msanii kutoka Nigeria, Seyi Shay akionyesha umahiri wake wakati wa onyesho maalum mara baada ya mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Viva Tower jijini Dar es Salaam.

Na Mwandisi Wetu

Balozi wa Pepsi aliyeibuliwa na baba'ake Beyonce
·    Akiri kuwazimia Alikiba, Christian Bella, ajipanga kupiga nao kolabo


FEBRUARI 10 mwaka huu, nyota wa muziki wa Afro-pop barani Afrika, Mnigeria Deborah Oluwaseyi Joshua 'Seyi Shay', alitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, tayari kwa shoo iliyofanyika Mwanza.

Seyi Shay, alikuwa mmoja wa nyota wa ndani na nje ya Tanzania, waliotumbuiza katika  Tamasha la Muzika Festival, lililofanyika katika Ufukwe wa Jembe 'Jembe Beach' kwenye mkesha wa Siku ya Wapendanao 'Valentine Day.' 

Hakuwa Seyi Shay pekee, bali kulikuwa pia na Mnigeria Augustine Miles Kelechi 'Tekno' wakiongozwa na wakali wa hapa nyumbani Juma Kassim 'Nature' na Omar Nyembo 'Ommy Dimpozi' waliopagawisha hasa mashabiki.

Wakali hao walifanya makubwa katika shoo hiyo, lakini wakapagawishwa zaidi na vitu adimu vilivyooneshwa na Seyi Shay, ambaye kabla ya ujio huo hakuwa na jina kubwa sana miongoni mwa mashabiki wa muziki nchini.

Baada ya shoo hiyo jijini Mwanza, Seyi Shay ambaye ni Balozi wa kinywaji baridi cha Pepsi, alirejea Dar es Salaam Februari 15 na kutembelea Kiwanda cha SBC Tanzania Limited, kilichopo Barabara ya Nyerere, kujionea uzalishaji.

Baada ya kufanya ziara hiyo, alihitimisha uwepo wake kwa kuongea na vyombo vya habari kwenye Ukumbi uliopo kwenye Jengo la Viva Tower, ambako aliwashukuru Watanzania kwa aina ya upendo waliomuonesha alipokuwa nchini.

"Naipenda Tanzania, kilichooneshwa na mashabiki kule Mwanza kimenifanya nitamani kurejea tena siku moja na kufanya onyesho. Najivunia ubalozi wangu wa Pepsi, kwani unanipa nafasi ya kutembelea nchi tofauti na kutanua sanaa yangu," alisisitiza.

Katika hafla hiyo ya kuwaaga Watanzania, Seyi Shay ambaye ni mshindi wa Tuzo za City People Entertainment 2013 alikoshinda kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Mwaka (wanawake), alipagawisha na vibao Right Now na Crays alichomshirikisha Wizkid.

Akiri kuwazimia Ali Kiba na Christian Bella

Katika hafla hiyo, Seyi Shay aliwamwagia sifa wasanii Ali Kiba 'Alikiba' na Christian Bella 'Obama' na kusema yuko katika hatua za mwisho kufanya nao kolabo, akitarajia kuanza na Alikiba Machi mwaka huu, kisha Bella baadaye.

"Ni wasanii wenye kila kitu kitu anachohitaji kuwa nacho msanii mzuri. Wana vipaji vya kuimba, wana sauti nzuri na kimsingi wanajua kutumia tunu hizo. Nimeongea nao na sasa niko katika hatua za mwisho kufanya nao kolabo.

"Mwezi ujao nitagharamia safari ya Alikiba kuja Nigeria kufanya kolabo, nikiamini kabisa itakuwa moto wa kuotea mbali, kutokana na uwezo alionao mkali huyo. Baada ya hapo nitaanza mchakato wa kumshirikisha Bella," alibainisha Seyi Shay.

Mkali huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, Tanzania ina utajiri wa wasanii mahiri, wenye vipaji vya hali ya juu, na kusema uwingi wao huo hauna athari kwa sanaa na wasanii husika, bali unafaida kwani unaongeza ushindani.

"Sanaa ni ushindani, uwingi wao haushushi thamani ya kazi zao, bali unachagiza. Wasanii wanapokuwa wengi, wanakuwa makini kutoa kazi nzuri ili kutoporomoka. Hata Nigeria iliyopiga hatua kwenye muziki na filamu, ilibebwa na hilo," alifichua.

Seyi Shay ni nani na ametokea wapi?

Mkali huyu alizaliwa Desemba 21, 1985, jijini London, England, kutoka kwa baba na mama raia wa Nigeria, mama yake akitokea Kaskazini na baba kutoka Kusini Magharibi mwa Nigeria, akiwa mtoto wa mwisho wa familia ya watoto wanne.

Nyota huyu wakati wa utoto wake alilelewa katika maadili ya kidini zaidi, ambako alionesha kipaji cha kuimba tangu akiwa na umri wa miaka sita, alikoimba kwaya kanisani na shuleni, akiwa mmoja wa washiriki wa awali wa Tamasha la London Community Gospel Choir.

Seyi Shay alianza kufanya muziki akiwa Chuo Kikuu cha East London, alikokuwa akisomea 'Business Management' na katika moja ya mahojiano yake kipinndi hicho aliwahi kukiri kuwa anajitosa katika muziki ambao mama yake hataki kumuona akifanya.

"Mama yangu ndoto zake zilikuwa ni kuniona nakuwa daktari ama mwanasheria, lakini ndoto zangu zilikuwa katika muziki, lakini kabla ya mama yangu kufariki, alinihusia kutoacha kumtukuza Mungu hata kama nimechagua muziki wa kidunia," alifichua nyota huyo.

Mafanikio yake katika muziki yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Mathew Knowles, ambaye ni baba wa mwanamuziki mahiri duniani, Beyoncé Giselle Knowles-Carter maarufu kama Beyonce, aliyemuona kupitia binti yake huyo.

Seyi Shay alionwa na kusaini mkataba wa kufanya kazi na Mathew Knowles, baada ya mzee huyo aliyekuwa pia Meneja wa binti yake, kuliona kundi la kina Seyi Shay wakiwa wadogo likitumbuiza katika ziara ya Beyoncé nchini Uingereza iliyoitwa I Am... World Tour.

Ni kupitia kipaji alichokionesha katika shoo hiyo, Mathew Knowles kupitia kampuni yake akamchomoa Seyi Shay kundi na kumuhamishia Houston, Marekani alikokuzwa kisanii na kuongezewa ubora unaompa heshima hivi sasa duniani.

Seyi Shay, amepitia mengi, akivuka milima na mabonde hadi kufikia kufanya kazi na wakali wa kimataifa kama Justin Timberlake, Brian Michael Cox, Darey, Bilal, Michelle Williams, Chip, Rob Knoxx, H-Money ma Cameron Wallace.

Ukiondoa Right Know na Crays, baadhi ya nyimbo alizotesa nazo katika tasnia ya muziki ni pamoja na Loving Your Way, No Le Le, Irawo, Irawo Remix aliyomshirikisha Vector), Chante aliofanya na Ajuju, Killin' Me Softly aliomshirikisha Timaya.

Nyingine ni pamoja na Chairman alioimba kwa kumshirikisha KCee, Ragga Ragga, Murda aliofanya na Patoranking na Shaydee, uliokuwamo katika albamu iliyokimbiza mno sokoni mwaka 2014, iitwayo Seyi or Shay na kibao kingine ni Jangilova.

Uwezo wa Seyi Shay unaweza pia kuthibitishwa kupitia nyimbo alizoshirikishwa na wasanii wengine, zikiwamo For You wa Praiz, Paradise wa Mr Walz, Get Down wa Yung GreyC, Yarinya wa Amir, In Love wa Wizkid, Sugar wa Ayoola na The Motion ya DJ Lambo.

Huyu ndiye Seyi Shay, mshindi wa Tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike Anayechipukia aliyochukua mwaka 2013, ikitolewa City People Entertainment.

No comments:

Post a Comment

Pages