HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 15, 2016

WAIMBAJI TAMASHA LA PASAKA WAZIDI KUMWAGIKA

 Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha Pasaka, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika mkoani Geita Machi 26.
 Alex Msama akifafanua jambo.
  
NA MWANDISHI WETU

IDADI ya waimbaji wa muziki injili watakaopamba tamasha la Pasaka, wamezidi kuongezeka baada ya wengine watatu wakiwemo wawili kutoka Kenya kuthibitisha ushiriki wao.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha hilo na Mkurugenzi wa Msama Promotions inayoratibu Tamasha hilo, Alex Msama amesema lengo lao ni kuona tukio hilo linakuwa na waimbaji wa kutosha.

“Tunashukuru, idadi ya waimbaji imezidi kuongezeka kwani wambaji wengine wawili kutoka Kenya na mwingine wa hapa nchini, nao wamethibitisha kushiriki tamasha hilo ambalo safari hii ni zamu ya Kanda ya Ziwa,” alisema Msama.

Msama amewataja waimbaji hao kutoka Kenya ni mwanamama Anastazia Mukabwa anayetamba na vibao mbalimbali kikiwemo cha ‘Vua Kiatu’ kilichompatia sifa kubwa ndani na nje ya nchi hiyo na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Mwingine aliyetajwa sambamba naye ni mwimbaji nguli Solomon Mukubwa, rais wa DR Congo mwenye maskani yake nchini Kenya akiungana na Faustine Munishi ‘Malebo,’ mtanzania anayeishi Kenya ambaye alikuwa wa kwanza kutajwa kutoka nchini humo.

Mbali ya waimbaji hao kutoka Kenya, Msama leo amemtangaza pia mwimbaji mwingine wa Tanzania, Jenifer Mgendi ambaye pia mbali ya kutamba na vibao mbalimbali vilivyomtambulisha, kwa sasa pia ni mcheza filamu.

Msama alisema tamasha hilo ambalo litaanza Machi 26 katika Ukumbi wa Desire wa mjini Geita, siku inayofuata itakuwa zamu ya wakazi wa jiji la Mwanza kupata uhondo huo katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Alisema kivumbi cha tamasha hilo kwa mwaka huu kitahitimishwa katika uwanja wa Taifa wa mjini Kahama na kutoa wito kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, kujitokeza kwa wingi.

“Nichukue nafasi hii kuwaeleza wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili hasa wa mkoa wa Kahama, Geita na Mwanza kwamba maandalizi ya Tamasha la Pasaka yanaendelea vizuri kwani waimbaji wamezidi kuthibitisha ushiriki wao,” alisema.

 Kwa upande wa malengo, Msama alisema ni kueneza ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya uimbaji katika kufurahia ushindi wa Krisho dhidi ya kifo na mauti, pia sehemu ya mapato ya kiingilio yatatumika kununua baiskeli kwa ajili ya wenye ulemavu.

Msama kupitia kampuni yake ya Msama Promotions ndie amekuwa akiratibu matukio ya muziki wa injili tangu mwaka 2000; wakati wa Sikukuu ya Pasaka na Krismas, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki huo kiasi cha kutoa ajira kwa vijana.

No comments:

Post a Comment

Pages