Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Makala (Picha Maktaba) |
Na EmanuelMadafa, Jamiimojablogu
SERIKALI Mkoani Mbeya imeagiza kufutwa kwa hati ya kiwanja
kilichotolewa na halmashauri ya Jiji la Mbeya kwenye chanzo kikuu cha maji
kilichopo eneo la Nyibuko kata ya Mwakibete kwa matumizi ya makazi.
Agizo hilo, limetolwa na Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya Amos Makala mara baada ya kutembelea na kukagua chanzo kikuu cha
maji cha Nzovwe, chenye uwezo wa kuzalisha mita 12 za ujazo kwa siku na
kusambaza maji kwa asilimia 41 kwa wakazi wa jiji la Mbeya wapatao zaidi
ya 200,000.
Kiwanja hicho ambacho kipo karibu na
eneo la chanzo cha maji cha Nzovwe, kilitolewa na maafisa ardhi, idara ya
mipango miji kwa ajili ya matumizi ya makazi na kumilikiwa na mtu binafsi
aliyetajwa kwa jina moja la Mwakasala.
Makala amesema, chanzo hicho cha maji ndio
tegemezi kwa kusambaza huduma ya maji kwa wananchi wa Jiji la Mbeya, hivyo kama
kitaachwa na kuharibiwa, wananchi zaidi ya 200,000 wapo hatarini kuikosa huduma
hiyo ambayo ni haki yao ya msingi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali iliwaondoa
wananchi wote waliokuwa wanaishi au kuendesha shughuli zao za kiuchumi ndani ya
mita 60 na kuwalipa fidia zao hivyo hatua ya wananchi hao kuendelea kuishia
mahali hapo ni kukaidi agizo la serikali.
Amebainisha kuwa kiwango kikubwa cha upotevu wa maji kwa asilimia 31 inatokana na baadhi ya vyanzo vya maji
kuharibiwa kwa kufanyika kwa shughuli za kibinadamu, kulisha mifugo au kujenga
nyumba za makazi pamoja na mabadiliko ya kihaidrolojia.
Hata hivyo, Mkuu huyo aliutaka
uongozi wa mamlaka ya maji kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa halmashauri ya
Jiji la Mbeya, kuhakikisha wanalisiamamia zoezi hilo la kumondoa mvamizi huyo
ndani ya siku tatu.
“Wananchi wengine wameondoka tena
kwa hiari yao wenyewe, sasa kwa nini huyu atuchezee mchezo mchafu? kwa hili
sikubaliani nalo, huku akiwataka wananchi ambao ni vijana kulilinda eneo hilo
na kuwaonya wale ambao watakubali kutumiwa na mtu au watu kufanya
fujo,”alisema.
No comments:
Post a Comment