Na Mwandishi wetu, Zanzibar
MWANAHARAKATI wa udhalilishaji wanawake na watoto, Zaituni Juma
(Mama Mkapa), ameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana nyumbani kwake
Bambi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Bi. Zaituni ambaye alikuwa
akifanya kazi bega kwa bega na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA),
alifikwa na mauti juzi, Jumamosi, Juni 26, 2016 majira ya jioni, alipokutwa
peke yake nje
ya nyumba yake na
kuvamiwa na wahalifu hao na kumpiga hadi kumtoa roho.
Akithibitisha kutokea kwa
tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Saad, alisema watu
wasiojuilikana mnamo majira ya jioni siku hiyo wakiwa wamefunika nyuso
walimvamia na kumkata mapanga hadi kumuua.
Alieleza kuwa tayari
wanamshikilia mtu mmoja ambaye anafanyiwa mahojiano ili kuthibitisha kama anahusika
au la, na kudai kwamba kwa sasa wanaendesha uchunguzi wao kwa siri ili kuwabaini
wahalifu.
“Unapoweka hadharani kila
kitu unaweza kuwafanya wengine wakimbie, kwa hiyo tunafanya hivyo kwanza hadi
tutakapowakamata wote,” alieleza Kamanda huyo wa Polisi wa Kusini Unguja.
Kufuatia tukio hilo Chama
cha Wanasheria Wanawake (ZAFELA) pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
(TAMWA) Zanzibar wanasikitika kupoteza mwanaharakati mkubwa wa masuala ya
kijinsia na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha
watuhumiwa wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mzuri Issa, ambaye ni Mratibu wa TAMWA Zanzibar alisema kuwa kifo cha
Zaituni ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupinga Ukatili wa
Kijinsia Mkoa wa Kusini Unguja (MKUKKU), kimekuwa pigo kubwa katika harakati za kupambana na vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia
pamoja na kutafuta usawa wa kijinsia kwa ujumla.
“Hili ni tukio la pili kumtokea
Zaituni katika kipindi cha miaka miwili, ambapo tukio la kwanza lilihusisha
kuvamiwa nyumbani kwake, kupigwa na kuibiwa fedha mwaka jana,” alieleza Mzuri.
Jamila Mahmoud, Mkurugenzi wa
ZAFELA, alisema wahusika wanatakiwa kusakwa
nakuchukuliwa hatua zinazostahili.
No comments:
Post a Comment