Ndugu
Waandishi wa Habari;
Tumewaita hapa leo ili tuwapatieni taarifa ya utekelezaji wa mpango wa
kuzuia simu bandia za kiganjani zisitumike kwenye mitandao ya simu hapa nchini.
Kama ambavyo mnakumbuka, usiku wa tarehe 16 Juni 2016 simu bandia
zilizuiwa kutumika katika mitandao ya simu. Maagizo ya Serikali kuzuia matumizi
ya simu bandia kwenye mitandao ni sehemu ya mpango wa kuanzishwa kwa rajisi kuu ya Namba
Tambulishi za simu za mkononi, kwa kifupi CEIR ambayo ni Central Equipment
Identification Register.
Uthibiti wa matumuzi ya simu
katika mitandao ya mawasiliano kunatokana na kuongezeka kwa umuhimu wa simu na
vifaa vya mkononi vya mawasiliano kama nyenzo muhimu kimaisha, kijamii,
kiuchumi, na kiusalama.
Vifaa vya mkononi vya mawasiliano ambavyo vinatumia laini ya simu, yaani
SIM card kuwasiliana vina namba maalum inayoitambulisha, ambayo inaitwa IMEI –
kifupisho cha International Mobile Equipment Identity.
Mfumo wa Rajisi
kuu ya Namba Tambulishi ni wa kielektroniki na
unahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya
mkononi (IMEI). Lengo la Rajisi ni kufuatilia namba
tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi
viwango (bandia) vya matumizi katika soko la mawasiliano.
Kuanzishwa kwa Mfumo
wa Rajisi kuu ya Namba Tambulishi kunatokana na matakwa ya kisheria,
ikiwemo masharti ya vifungu vifungu vya 84 hadi 90 vya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010 na Kanuni za
Namba Tambulishi (Central Equipment Identity Register) za mwaka 2011. Sheria na Kanuni vinaipa Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania nguvu ya kusimamia kwa karibu vifaa vya kielektroniki
vya mawasiliano vyenye namba tambulishi.
Sheria
na Kanuni hizi zinawataka watoa huduma za simu za kiganjani kuwa na Mfumo wa ndani wa Rajisi ya Namba za
Utambulisho wa simu za kiganjani yaani ‘Equipment Identity Register’ kwa kifupi EIR katika mitandao yao. Mifumo hii
imeunganishwa na Rajisi Kuu iliyoko hapa TCRA.
Aidha
Sheria inawataka watumiaji kusajili IMEI za vifaa wanavyotumia.
Mfumo
huu una faida zifuatazo:-
·
Kuongeza usalama mtandaoni kwa watumiaji wa simu, kwani simu zote za
kiganjani zitakuwa zinajulikana;
·
Kuzuia matumizi ya simu zisizokuwa na viwango hivyo kuepuka madhara
yatokanayo na simu zisizokuwa na ubora stahiki;
·
Kuthibiti wizi wa simu.
Iwapo mtu atapoteza au ataibiwa simu ya kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa
huduma, simu hiyo tafungiwa isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa
simu za kiganjani;
·
Kuhimiza utii wa sheria:
Kifungu cha 128 cha EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea
au kuibiwa kwa simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya
simu kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu.
·
Kujenga misingi ya matumizi
ya simu halisi, zisizo bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo
inakidhi viwango, ni halisi na sio bandia.Hii pia itatoa fursa kwa wateja wa
simu za kiganjani kupata bidhaa inayolingana na pesa walizotoa kununulia simu
hizo.
Uzimaji wa
Simu
Usiku wa manane tarehe 16
Juni, 2016 simu ambazo zilikuwa hazina viwango (bandia) zilizimwa kwa
kuzingatia uchambuzi wa kina uliofanyika ili kubaini namba tambulishi ambazo hazikuwa na viwango. Namba
tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango ilikuwa ni asilimia 2.96 ya simu
zilizokuwa zinatumika kwenye mitandao ya makampuni ya simu hapa nchini. Simu
zilizokuwa na namba tambulishi ambazo zimenakiliwa, yaani duplicates zilikuwa
asilimia 0.09 na asilimia
96.95 ilikuwa ni idadi
ya namba tambulishi za simu halisi (genuine).
Hadi kufikia sasa idadi ya namba tambulishi ambazo hazikidhi
viwango zimefikia 1,713,337.
Baada ya
kukamilika kwa zoezi la kuzimwa kwa simu zenye namba tambulishi ambazo hazikuwa
za viwango (invalid IMEIS) na namba tambulishi zilizonakiliwa (Duplicate IMEIs)
hadi sasa idadi ya namba tambulishi zilizonakiliwa ambazo zimezimwa imefikia 117,389.
Uelewa wa wananchi umechangia kwa
kiasi kikubwa katika kufanikisha mpango huu.
Kama mnavyokumbuka, Mamlaka ya
Mawasiliano iliratibu na kuendesha mpango wa elimu kwa umma kuhusu rajisi kuu
ya namba tambulishi nchini kote na kupitia vyombo vya habari kati ya 17 Desemba
2015 na 16 Juni 2016.
Katika kutelekeza mpango huu,
tumekumbana na changamoto zifuatazo:-
- Uaminifu mdogo kwa baadhi ya wauzaji wa simu kwa
kutoa punguzo kwa wananchi ili kuwashawishi kuzinunua simu bandia kwa bei
nafuu. Hata hivyo ni jambo la kutia moyo kwamba wananchi wengi hawakubali
kudanganywa.
- Gharama zinazohitajika katika kuwafikia wananchi na
kuelimisha ili waweze kuelewa zaidi juu ya mpango mzima wa kuhakiki simu
zao. Tanzania ni kubwa na hatukuweza kufika kila mahali kutokana na ufinyu
wa bajeti.
- Baadhi
ya watumiaji kutokufuata maelekezo
ya namna ya kuhakiki simu zao katika kipindi cha mpito. Kwa mfano, wengi
walikuwa wanakosea kutuma ujumbe wenye Namba tambulishi kwenda 15090.
- Baadhi
ya watumiaji kuamini kwamba simu bandia ni zile za bei rahisi au ambazo
zimenunuliwa hapa nchini na hivyo kulalamika walipofungiwa simu walizonunua kwa bei kubwa na ambazo
ni bandia.
- Baadhi ya watoa huduma kushindwa
kushughulikia malalamiko ya wateja waliofungiwa simu zao kwa wakati.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
inaendelea kuwakumbusha watanzania wote kuwa ni jukumu la kila mmoja
kuhakikisha kuwa simu yake ni halisi na sio bandia. Pia wananchi wanakumbushwa kutoshikilia simu
zilizozimwa majumbani na kuzipeleka mahali husika kwa ajili ya ukusanyaji
(disposal).
Vilevile
Mamlaka inawakumbusha wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi na mafundi
simu kuwa ni kosa kubadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mkononi
(mobile devices). Kwa mujibu wa kifungu cha 127 cha Sheria ya Mawasiliano ya
Kielektroniki na Posta (EPOCA), mtu yeyote ambaye anachakachua simu au lani ya
simu kwa lengo la kubadilisha uhalisia wake anatenda kosa ambalo adhabu yake ni
faini isiyopungua shilingi millioni 30 au kifungo kisichozidi miaka kumi (10)
au vyote kwa pamoja.
Aidha, kifungu
cha 135 cha EPOCA kimeweka adhabu ya faini ya shilingi 1,500,000 au kifungo cha
miaka mitano au vyote kwa pamoja kwa matu ambaye anachakachua simu iliyofungiwa.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inatoa
wito kwa wale wote wote wanaofanya biashara za kuingingiza simu hapa nchini
kutoka nje wahakikishe kuwa simu wanazoleta zinakidhi viwango, zimehakikiwa kwa
mujibu wa wa Shirika la Viwango Tanzania.
Aidha Mamlaka
inawakumbusha kwa mara nyingine kuwa wanapaswa kuwa na leseni ya Mamlaka ya
Mawasiliano kwa mujibu wa Sheria. Hii pia ni kwa mafundi wote wa simu nchini,
wanatakiwa kuanza mchakato wa kupata leseni ya kutengeneza simu, ikiwa ni
pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaorodhesha wanaoleta simu zao kutengenezwa ili
kuepuka kuwa sehemu ya mtandao wa wizi wa simu.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
inawashukuru wadau wote walioshiriki katika kufanikisha Mpango huu. Hao ni
pamoja na makampuni ya simu za mkononi, jeshi la Polisi, Viongozi wa mikoa
ambako elimu kwa umma ilitolewa, vyombo vya habari Tume ya Ushindani (FCC)
pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Asanteni.
IMETOLEWA
NA KAIMU MKURUGENZI MKUU, MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
4 JULAI,
2016


No comments:
Post a Comment