HABARI MSETO (HEADER)


August 03, 2016

NMB AgriBiashara yazinduliwa Dar


Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussmaker akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa huduma mpya katika sekta ya kilimo na ufugaji. Uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Renatus Mushin na Ofisa Mwandamizi Kilimo Biashara NMB, Saif Ahmed. (Picha na Francis Dande)

  Na Mwandishi Wetu

BENKI ya NMB, jana imezindua huduma mpya itakayohudumu katika sekta ya kilimo na ufugaji ndani ya nchi, ijulikanayo kwa jina la NMB AgriBiashara.

Huduma hiyo ilizinduliwa Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam, ikilenga kutoa huduma kwa wadau wa sekta hiyo miongoni mwa wateja wa zamani na wateja wapya wa NMB.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussmaker, alibainisha kuwa AgriBiashara ni huduma iliyotengewa kiasi cha Sh. Bil. 500 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alibainsiha kuwa, kupitia AgriBiashara, wadau wa sekta ya kilimo na ufugaji watanufaika na huduma hiyo kupitia Mkopo wa Stakabadhi Ghalani na Mkopo wa Kilimo cha Mkataba.

Pia kutakuwa na Mkopo wa Muda Mfupi, Kati na Mrefu, sambamba na Akaunti Maalum za AgriBiashara, hivyo kuwawezesha katika shughuli zinazohusiana na kilimo na ufugaji.

"Kupitia AgriBiashara, wateja wapya na wale wa zamani wa NMB, watawezeshwaa kupata huduma za mikopo ya pembejeo, ukulima, mazao, uchuuzi, usindikaji na usambazaji thabiti, bora na wa kisasa zaidi," alisema Ineke.
Alifafanua kuwa, wataalamu wa NMB wamesambazwa kote nchini, kuhudumia wadau wa kilimo, biashara na ufugaji, huduma ambazo hupatikana kwa mtu mmoja mmoja na vikundi, kwenye matawi yote ya Tanzania.

Aliyataja baadhi ya mazao watakayojihusisha nayo kuwa ni korosho, kahawa, pamba, miwa, mpunga, alizeti, mbogamboga, mahindi, tumbaku, ufuta, matunda, maua, na mazao ya mifugo kama maziwa na nyama.

Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Renatus Mushi, alibainisha kuwa, huduma hiyo ya AgriBiashara ilikuwapo, ingawa ilihudumu katika mazao machache, lakini sasa imeboreshwa na imekuja kuikomboa sekta ya kilimo.

Alibainisha kuwa, AgriBiashara inahusisha mnyororo mrefu wa thamani (value chain), uliobeba ukombozi katika sekta ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa Tanzania kama taifa.

No comments:

Post a Comment

Pages