WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuweka mikakati
endelevu ya kuwawezesha wananchi kuvua katika maji ya kina kirefu cha bahari
kwa kutumia meli kubwa na za kisasa ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo
ambayo imekuwa ikichukuliwa na wavuvi wenye vyombo vya kisasa kutoka nje ya nchi.
Aidha,
amezitaka halmashauri zote nchini ziweke mikakati na mipango ya kuifanya mito
na maziwa mbalimbali nchini kuwa na uvuvi endelevu kwa kufuatilia kwa karibu shughuli
za wavuvi na kuwaadhibu wote watakaovua kinyume na sheria.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Agosti 01, 2016) wakati akifungua maadhimisho
ya 23 ya sherehe za maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki katika Uwanja wa Mwalimu
J.K Nyerere yanayofanyika katika mkoa wa Morogoro ambapo amesema bado nchi haijaweza
kutumia rasilimali hiyo kikamilifu.
Amesema
halmashauri zinatakiwa zihamasishe vijana kuunda vikundi vya kuanzisha miradi
ya kufuga samaki katika maeneo yao na wewezeshwe kupata teknolojia ya ufugaji
huo.
Akizungumzia
vikundi vya wajasiariamali wanaovua katika maeneo ya bahari na maziwa alishauri
waelimishwe kuhusu namna ya kupata mikopo ya kununulia zana bora za kisasa za
uvuvi ili shughuli zao ziwe na tija.
Katika hatua nyingine
Waziri Mkuu amesema wakulima wanatakiwa kuzingatia matumizi ya kanuni bora za kilimo
ikiwemo matumizi sahihi ya zana za kisasa, pembejeo na viuatilifu vilivyopendekezwa
na wataalam ili kufanikisha mapinduzi ya kilimo kuelekea kilimo cha biashara.
Akizungumzia
kuhusu suala la usindikaji alisema wakati anatembelea mabanda mbalimbali
alipata fursa ya kuona teknolojia zinazoweza kutumiwa na wakulima, wafugaji na
wavuvi katika kuongeza uzalishaji bora wenye tija.
Amesema
amefurahi kuona wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wa mazao, pembejeo na
zana za kilimo wana ari kubwa ya kushiriki katika kuleta mapinduzi katika sekta
ya kilimo ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya kuifanya nchi
kujitosheleza kwa chakula na kuendeleza uchumi wa viwanda.
“Naamini
kuwa pamoja na lengo la kujitosheleza kwa chakula, wakulima, wafugaji na wavuvi
wataongeza ari ya uzalishaji kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi
katika kuvipatia viwanda vyetu malighafi na kuongeza thamani ya mazao,”
alisema.
Kufuatia
hatua hiyo Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote kuhamasisha uanzishaji na
uendelezaji wa viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi
kwa kushirikisha taasisi za umma na binafsi, mashirika na vikundi vya
ujasiriamali katika maeneo yao.
Akizungumzia
namna Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya wafugaji
na wakulima Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi watahamishiwa
katika vitalu vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye mifugo michache
watatengewa maeneo katika vijiji.
Awali
Waziri Mkuu alitembelea baadhi ya mabanda na maeneo ya vipando vya mazao mbali
mbali yaliyoko katika viwanja hivyo ambapo alisema ameridhishwa na juhudi zilizofanyika
katika maandalizi ya maonesho ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa uwanja
huo.
“Napenda
kutoa pongezi za dhati kwa kujenga miundombinu na nyumba za kudumu za kufanyia
maonesho. Aidha, natoa shukrani za pekee kwa Halmashauri zetu, Mashirika yetu
ya Umma na binafsi; na watu binafsi ambao wamejenga na wanaendelea kujenga
majengo mazuri na ya kudumu,” alisema.
Pia
alizindua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Temeke na kusema kuwa uboreshaji wa
viwanja hivyo unaonesha jinsi wadau wote katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi
na ushirika wanavyotambua umuhimu wa maonesho hayo kama njia ya kuongeza
maarifa na kumuenzi mkulima, mfugaji na mvuvi kwa kutambua mchango wao katika
uchumi wa Taifa.
Kauli
mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni kilimo,
mifugo na uvuvi ni nguzo ya maendeleo: vijana shiriki kikamilifu
(“HAPA KAZI TU”)
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
AGOSTI 01, 2016.
No comments:
Post a Comment