HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 05, 2017

Diwani Assenga awakumbuka Jellah Mtagwa, Peter Tino

Na Mwandishi Wetu

WACHEZAJI nembo ya Tanzania Kimataifa wanatarajia kuzindua mashindano ya kuwania kombe la Diwani wa Kata ya Tabata, Patrick Assenga (Chadema) yanayotarajia kuanza (Kesho-Jumamosi) mwishoni mwa wiki kwenye uwanja wa Shule ya msingi Tabata.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa kwa timu shiriki za mashindano hayo, Assenga alisema wachezaji wanaotarajia kuwa sehemu ya uzinduzi wa mashindano hayo ni pamopja na Jellah Mtagwa, Peter Tino, Dua Said, Moses Mkandawile na wengineo waliowahi kuitangaza nchi nje ya mipaka yake.

“Tumepanga wachezaji wa zamani watacheza kwa dakika chache katika uzinduzi wa mashindano hayo na baadaye tutawakabidhi zawadi maalum kwa lengo la kuthamini mchango wao katika soka la Tanzania,” alisema Assenga.

Assenga alisema katika mashindano yake yanayotarajia kushirikisha timu 16 za mitaa nane iliyoko katika kata hiyo, ameguswa na wachezaji waliowahi kutamba katika soka la Tanzania ambao hawathaminiwi kama mashujaa waliofanya makubwa katika nchi hii.

Assenga alisema uandaaji wa mashindano hayo ni ahadi aliyowahi kuitoa wakati wa kampeni za kuwania uongozi huo  kwamba atajikita zaidi kwenye kusaidia vijana hasa katika upande wa michezo na maendeleo mengine yanayowahusu vijana.

Diwani huyo alisema pamoja na kuwa na lengo la kuwasaidia vijana pia kuwapa thamani waliokuwa wachezaji waliowahi kuitangaza Tanzania katika nchi nyingine kama Nigeria, Liberia na kwingineko.

Aidha Diwani huyo alisema mashindano hayo yatakuwa yakifanyika kila mwaka hadi atakapomaliza uongozi wake katika Kata  hiyo ambako katika uzinduzi huo, Meya wa Ilala Charles Kuyeko anatarajia kuwa mgeni rasmi.

“Nimepanga pia kabla ya kuanza mashindano, Jumamosi nitashirikiana na na wananchi wa Tabata kufanya usafi  kwa kushirikiana na wananchi wa Kata hiyo, hivyo nawaomba wakazi wa Tabata kujitokeza kufanya usafi katika maeneo yao,” alisema Assenga.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya mashindano hayo, Rogers Peter alisema  wamejipanga vilivyo kufanikisha mashindano hayo ambayo yanabeba taswira ya Tanzania kwa sababu wamekumbuka wachezaji  wa zamani na  kuwalinganisha na vijana  wa sasa lengo likiwa ni kutoa elimu kwa vijana na kuwatengenezea fursa zaidi kwa ajira.

Hata hivyo, Peter alitumia fursa hiyo kumuomba Diwani kutupia macho fursa nyingine za mchezo kkwa upande wa soka la ufukweni na wanawake akiwa na dhamira ya kutaka Tabata kuwa kisima cha vipajia nchini.

Naye Mkuu wa Nidhamu wa mashindano hayo, aliyekuwa golikipa wa Simba, Moses Mkandawile alisema katika historia ya Tabata haijawahi kutokea kiongozi mwenye maono kama Assenga ambaye ameguswa zaidi  na vijana ambao  mara nyingi wanashinda vijiweni.

No comments:

Post a Comment

Pages