Na Theresia Mwami, TEMESA
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Iddi Mgwatu leo
amefungua mafunzo elekezi kwa mameneja wa mikoa na vituo vya TEMESA juu ya tozo
za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo pamoja na uaandaji wa taarifa za
uzalishaji za mwezi kwa watumishi wa TEMESA kutoka katika mikoa na vituo mbali
mbali vilivyopo nchini.
Katika
hotuba yake Dkt. Mgwatu amewataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanashiriki
mafunzo hayo kwa umakini mkubwa ili kuleta mabadiliko chanya kwa TEMESA na
kuondoa kero mbalimbali zilizopo sasa, ikiwemo kero ya gharama kubwa za
matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya serikali na kuwataka watumishi
hao kuondokana na wazabuni wanaouza vipuri na vilainishi vya magari kwa bei ghali
isiyo ya soko.
“Mafunzo
haya ni gharama na kwa hiyo haitakuwa jambo jema tukarudi katika vituo vyetu na
kuendeleza mambo yale yale kwa mazoea. Tutakuwa hatujatenda haki kwa wananchi
na kwa taifa kwa ujumla. Niwe mkweli kuwa nitachukua hatua kali pale
nitakapoona mkoa au kituo hakifanyi vyema katika utendaji kazi wake” alisema
Dr. Mgwatu.
Nae
Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Matengenezo Mhandisi Sylvester Semfukwe amesema
kuwa idara yake imeandaa mada mbali mbali kwa ajili ya mafunzo hayo zikiwemo:
Tozo ya matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo kwa kuzingatia muda halisi
wa matengenezo, Mfumo mpya wa kuandaa taarifa za uzalishaji za kila mwezi,
Namna ya kubaini vipuri bandia kwa njia ya kielektroniki, Masuala ya masoko na
huduma kwa mteja pamoja na mwongozo wa uwandaaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18.
Mafunzo
hayo ya siku tano yaliyoanza jana katika Ukumbi wa TBA mkoani Dodoma,
yanashirikisha jumla ya mikoa 19 yenye vituo vya TEMESA, yanatarajia kukamilika
Ijumaa tarehe 20/01/2017. Aidha mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo kama hayo
yaliyofanyika mwezi Desemba, 2016 mkoani Dar es Salaam na yalishirikisha mikoa
sita.
No comments:
Post a Comment