Dodoma, Jumatatu, Januari 30, 2017:
Katika toleo la Jumatatu, Januari 30-Februari 5, 2017 gazeti
la MwanaHALISI linalochapishwa na
kampuni ya Hali Halisi Publishers LTD kumechapisha habari kuu katika
ukurasa wa kwanza inayosomeka “Ufisadi
ndani ya ofisi ya JPM.”
Licha
ya habari hiyo kujenga dhana kuwa Rais John Pombe Magufuli anahusika na
kilichoitwa ufisadi, msingi wa taarifa husika ni tatizo la manunuzi katika
Shirika la Elimu Kibaha!
Kwa
kuwa ni jambo lililodhahiri kuwa Shirika la Elimu Kibaha si ofisi, idara wala
kitengo “ndani ya ofisi ya JPM”
mwandishi na mhariri wa habari husika wamedhihirisha malengo ya kumchafua Rais binafsi
kwa jamii.
Aidha,
katika siku za karibuni Serikali imejitahidi kufanya mazungumzo na wahariri wa gazeti
hili kwa lengo la kukumbushana maadili ya uandishi wa habari, ni bahati mbaya kwamba
wamekuwa wakikaidi japo wito tu.
Kwa
sababu hizi, Serikali inawaagiza wahariri wa gazeti hilo kujitathmini na
kuchukua hatua kwa kutumia kifungu cha 40 cha Sheria ya Huduma za Habari, 2016 kinachowapa fursa ya kuomba radhi,
kwa kumuomba radhi Rais ndani ya saa 24 kuanzia saa 10 jioni ya leo Januari 30,
2017.
Iwapo
wahusika wataona muhali kufanya hivyo, Serikali itachukua hatua kali kwa mujibu
wa sheria na masharti ya usajili ya gazeti husika. Tunaendelea kuwashukuru
wanahabari wanaofuata maadili ya taaluma.
Imetolewa
na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO
No comments:
Post a Comment