Na Hassan Silayo, MAELEZO
Tatizo la ongezeko la idadi ya vijana na watu wazima waliokosa elimu ya sekondari ni kubwa sio tu hapa Tanzania bali ni kwa nchi zote za kusini mwa jangwa la sahara, Kwa mfano, kwa takwimu za sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina jumla ya vijana wa umri wa miaka 7-17 milioni 3.5 ambao wapo nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Hii hufanya vijana milioni 2.5 kuhitaji elimu ya sekondari na wengine milioni 1 kuhitaji elimu ya msingi na ukweli ni kwamba vijana wanaomaliza elimu ya msingi na kupata alama za ufaulu chini ya 100 (kati ya 250) wamekuwa wakiachwa bila kwenda sekondari katika Mikoa mbalimbali isipokuwa wale ambao wazazi/walezi wao wanauwezo wa kuwapeleka kwenye shule za sekondari za binafsi ambazo gharama zake ni za juu.
Takwimu za sensa ya mwaka 2012 zinaonesha kuwa kufikia mwaka 2015 idadi ya vijana walio nje ya shule itaongezeka kufikia milioni 5.
Ili kukabiliana na tatizo hili, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilianzisha programu ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi mwaka 1992 ili kutoa fursa ya elimu ya sekondari kwa vijana na watu wazima waliokosa nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali.
akiongea kuhusu programu hiyo Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima Dkt.Kassim Nihuki alisema Programu inawalenga wanafunzi waliomaliza darasa la saba ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari na wale ambao kwa sababu moja au nyingine hawakumaliza elimu ya sekondari na wanataka kumaliza elimu hiyo.
Dkt. Nihuki aliongeza kuwa programu hii pia inawalenga wanafunzi ambao wamemaliza masomo ya MEMKWA (mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa) na wale wamemaliza masomo ya sekondari lakini hawakufanya vizuri na wangependa kurudia mtihani wa Taifa wa kidato cha nne pamoja na wafanyakazi wa serikali na sekta binafsi ambao hawana elimu ya sekondari na wanatakiwa wawe na kiwango hicho cha elimu.
Dkt Nihuki anasema kuwa masomo katika programu hii yanatolewa katika hatua tatu kubwa ikiwa hatua ya kwanza inabeba masomo ya kidato cha kwanza na chapili huku hatua ya tatu ikibeba masomo ya kidato cha tatu na nne na hatua ya tatu inabeba masomo ya kidato cha tano na sita.
Naye Mkuu wa Idara ya Elimu Msafa Bw. Baraka Kionywaki amesema kuwa Katika hatua ya I, mlengwa anasoma kwa kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa maarifa (yaani “Qualifying test”).
Bw. Kionywaki aliongeza kuwa jumla ya masomo 7 ya lazima yanayotolewa katika hatua hii ambayo ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kiswahili, Hisabati, Biolojia na Uraia (Civics). Aidha, mlengwa anaweza kuchagua masomo ya ziada ya sayansi au biashara kwa kadri atakavyoona inafaa. Mlengwa wa hatua ya II anasoma kwa kipindi cha mwaka mwingine mmoja na hivyo kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne unaoandaliwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Katika hatua ya tatu mlengwa atasoma kwa kipindi cha mwaka mwingine mmoja na hivyo kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha sita unaoandaliwa na NECTA. Ambapo katika hatua hii, masomo yanatolewa katika tahasusi (“combinations”) za HGL (Historia, Jiografia na Lugha), HKL (Historia, Kiswahili na Lugha), HGK (Historia, Jiografia na Kiswahili) na HGE (Historia, Jiografia na Uchumi). Hata hivyo mlengwa katika kila hatua anaweza kusoma kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi pale atakapokuwa amejiandaa kiasi cha kutosha kufanya mtihani wa maarifa au ule wa NECTA.
Katika hatua zote, masomo yanatolewa kupitia mafunzo ya ana kwa ana ya jioni (evening programme) kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 12 jioni pamoja na kujisomea moduli na vitabu na matumizi ya teknolojia za kujifunzia kama vile “CDs” na elimu mtandao (e-learning) yakiwemo machapisho huria ya kielimu (open educational resources).
Programu hii ambayo inaendeshwa katika majengo ya shule za msingi na sekondari za serikali 83 na shule za wadau mbalimbali 337 nchini zimewanufaisha vijana na watu wazima 95,140 (wanawake 61049 na wanaume 44893) katika mikoa mbalimbali kwa kipindi cha tangu mwaka 2010 hadi 2016.
Vijana na watu wazima wana budi kuendela kutumia fursa hii ili kuweza kupata elimu ya sekondari pamoja na kuziomba mamlaka za serikali za mitaa kuwahimiza wazazi/walezi kuwapeleka vijana wao waliokosa alama za ufaulu katika mtihani wa darasa la saba kutumia fursa ya elimu kupitia Taasisis ya Elimu ya Watu Wazima
No comments:
Post a Comment