Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Januari Makamba
(katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa agizo la
kupiga marufuku uzalishaji na uuzaji wa pombe aina ya viroba leo Jijini Dar es
Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na
Muungano Profesa Faustine Kamuzora na Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi hiyo
Richard Muyungi. Picha na:
Frank Mvungi – MAELEZO.
Na Frank Shija-MAELEZO
SERIKALI imepiga rasmi marufuku
matumizi ya pombe zinazofungashwa katika vifungashio vya plastiki maarufu kama
viroba kuanzia tarehe 1 Machi 2017.
Hayo yamebainishwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano Januari Makamba wakati
akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
“Dhamira ya Serikali siyo kupiga
marufuku vinywaji vya pombe kali bali ni kutekeleza Ibara ya 14 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 ambayo inatoa haki ya kuishi katika
mazingira yaliyo safi, salama na yenye afya,” alisema Makamba.
Aliongeza kuwa uamuzi huo
wakusitisha matumizi ya pombe hizo, Serikali itatumia Sheria ya Mazingira ya
mwaka 2004 ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza utaratibu wa utekelezaji wa
maamuzi hayo.
Alizitaja taratibu hizo kuwa ni
pamoja na kutungwa kwa kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio vya
plastiki kwa mujibu wa kifungu 230 (2) (F) CHA Sheria ya mazingira ya 2004.
Aidha Waziri Makamba ametoa wito
kwa wazalishaji wa pombe kali wanaohitaji muda wa ziada wa kuhamia katika
teknolojia ya chupa kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya kupewa kibali cha
kuendelea na uzalishaji huku wakihama kabla ya tarehe 28 Februari.
Makamba alisema kuwa maombi hayo
yaambatanishwe pamoja na ushahidi wa barua ikionyesha mwenendo wa ulipaji wa
kodi, nyaraka kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA) kuhusu usalama wa
kinywaji, uthibitisho wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS),cheti cha tathmini ya
athari za mazingira, uthibitisho kuwa atatumia teknolojia ya kudhibiti
utengenezaji wa vifungashio bandia na uthibitisho kutoka Wakala wa Usajili wa
Biashara na Leseni.
Katika hatua nyingine Waziri
Makamba amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini kuendesha operesheni kwa ajili ya
kudhibiti uingizwaji wa pombe kali zinazotoka nje na kuzuia matumizi ya pombe
haramu aina ya Gongo.
Utekelezaji wa uamuzi huo
unafuatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kusitisha matumizi ya
vifungashio vya plastiki ikiwemo pombe za viroba iliyotolewa bunge mwezi Mei
2016, Agosti na Desemba 2016 na kufuatiwa na agizo la Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa Majaliwa akiwa ziarani mkoani Manyara aliagiza kusitishwa kwa
utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zunazofungashwa kwenye vifungashio
vya plastiki kuanzia tarehe 1 Machi.
No comments:
Post a Comment