HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 07, 2017

Watakaong’ara Mbio za Taifa Moshi, kuiwakilisha Tz Mbio za Nyika Dunia

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limetangaza zawadi za washindi wa Mashindano ya Riadha ya Taifa yatakayofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro, ambako watakaofanya vema watafuzu kwa Mashindano ya Mbio za Nyika za Dunia (World Cross Country).

Mashindano ya Taifa yatafanyika Februari 18 mwaka huu, mwezi mmoja kabla ya kurindima kwa Mbio za Nyika za Dunia, jijini Kampala nchini Uganda, ambako RT tayari imeshaanza maandalizi tangu Desemba mwaka jana ili kufanya makubwa mashondanoni.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaa, Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday, alisema shirikisho lake linaamini kuwa timu za wakubwa na wadogogo zitapatikana kutokana na maandalizi hayo, ili washindi watakaofuzu waingie kambini kuelekea Uganda.

Gidabuday alibainisha ya kwamba, Tanzania inategemea kupeleka washiriki 28 nchini Uganda, ambayo ni idadi kuu inayotakiwa, na kwamba kutakuwa na timu tano ambazo ni Wanawake Seniors Km 10, Wanawake Juniors Km 6 na Wanaume Juniors Km 8, Wanaume Senior Km 10.

Aliongeza kuwa, Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), limeanzisha mashindano mapya ya ‘Relay’ ambayo yatakuwa na idadi ya wanariadha wanne, wawili ni wanawake na wawili ni wanaume, ambayo pia timu yake itakuwa moja kati ya hizo tano.

Alizitaja zawadi za Mashindano ya Taifa kuwa ni mshindi wa kwanza kila mbio Sh. 400,000, wa pili Sh. 300,000, wa tatu Sh. 200,000, wa nne Sh. 100,000, wa tano Sh. 90,000, wa sita Sh. 80,000, wa saba Sh. 70,000, wa nane Sh. 60,000, wa tisa Sh. 50,000 na wa 10 ni Sh. 40,000. 

Gidabuday aliongeza ya kwamba, jumla ya zawadi zitakazotolewa siku hiyo kwa washindi ni zaidi ya Sh. Mil 5.5, huku akitumia muda huo kuwaomba wadau na serikali kuiunga mkono RT katika kufanikisha mashindano ya Taifa na ushiriki wa Mbio za Dunia Kampala.

“Wakati Alphonce Felix Simbu alipopokelewa baada ya kushinda Mbio za Standard Chartered Mumbai kule India, Serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, iliahidi kutia mkono, wakati ndio huu sasa kutusapoti,” alisema Gidabuday. 

Alimaliza kwa kutoa wito kwa wakazi wa Moshi na vitongoji vyake, kujitokeza kwa wingi kwenye Viwanja vya Gofu kushuhudia mashindano hayo yatakayokuwa na msisimko wa kipekee, ambayo yatatoa wawakilishi watakaopeperusha Bendera ya Tanzania huko Uganda.

No comments:

Post a Comment

Pages