Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeukosoa upande wa serikali katika kesi ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo inayowakabili watu sita akiwemo mfanyabiashara Yusuf Ali (34) ‘Mpemba wa Magufuli’ kutowapa lugha tamu washtakiwa kuwa upelelezi umekamilika.
Hatua hiyo ilitokana na upande huo wa serikali kuieleza mahakama hiyo kuwa jalada la kesi hiyo bado lipo kwa Mkuu wa upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi (RCO) kwa ajili ya kuandaliwa ili lipelekwe kwenye Mahakam Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ‘Mahakama ya Mafisadi’.
Jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliutaka upande huo kuacha kuzungumza lugha tamu zinazowapa matumaini washtakiwa badala yake wanyooshe maelezo kwamba upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Awali, Wakili wa Serikali, Elia Athanas alidai kuwa kesi imeitishwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba jalada la kesi hiyo lipo kwa RCO ambaye anaandaa vijalada mbalimbali ili kupelekwa Mahakama ya Mafisadi.
Aliomba mahakama iendelee kurekodi kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika licha ya awali kudaiwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika. Hivyo aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Utetezi, Nehemiah Nkoko alidai kuwa upande wa mashitaka unatakiwa kuwapa msisitizo RCO wamalize vijalada mapema ili kesi hiyo ipelekwe Mahakama ya Mafisadi kama ulivyosema upande wa serikali.
Pia alidai, upande huo wanaposema kuwa upelelezi haujakamilika wakati tayari mawakili wengine walidai kuwa upelelezi umekamilika, wanarudisha nyuma kesi hiyo ambayo imepiga hatua kubwa.
Aidha, Wakili Josephat Mabula alidai kuwa upande wa mashitaka umekuwa na kauli kinzani na ukweli ni kwamba upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo wanatakiwa kuwa na kauli moja.
Hakimu Simba alisema kuwa si kweli kwamba baada ya kutengeneza vijalada kesi hiyo inapelekwa Mahakama ya Mafisadi bali inaenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) ambaye ataandaa maelezo ya mashahidi na ambayo baada ya kusomewa ndio itaelezwa kama kesi itasikilizwa mahakamani hapo au la.
"Upande wa mashitaka acheni kutoa lugha tamu tamu ambazo zinawapa washitakiwa matumaini. Mpaka RCO aseme kwamba wametengeneza hivyo vijalada kwenda mahakama ya mafisadi basi upelelezi utakuwa umekamilika lakini ninachoomba upelelezi ukamilishwe," alisema Hakimu Simba.
Pia alisema kuwa upande huo wanapoendelea kutoa lugha za nafuu itawapa mwanya upande wa utetezi hivyo wanapaswa kuwa na lugha iliyonyooka ili kufuata taratibu zilizowekwa.
Hata hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi February 21 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Mbali ya Yusuf, washtakiwa wengine ni Charles Mrutu (37) mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa (40) mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima (30) mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo (33) dereva na Pius Kulagwa (46) wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh.milioni 785.6.
Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, mwaka huu wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh milioni 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Katika shitaka la pili inadaiwa kuwa, Oktoba 26, mwaka huu, wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo va uzito wa kilo 13.85 vya thamani ya dola za Marekani 30,000 (Sh milioni 65.4).
Katika mashtaka mengine, inadaiwa Oktoba 27, mwaka huu, wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vya uzito wa kilo 11.1 na thamani ya dola za Marekani 15,000 (Sh milioni 32.7).
Aidha, Oktoba 29, mwaka huu walikutwa na vipande 36 vya thamani ya Sh milioni 294.6 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
No comments:
Post a Comment