HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 07, 2017

WEMA BADO ASOTA RUMANDE, WENGINE WAPATA DHAMANA

 Baadhi ya wasanii wakiwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kabla ya kupanda kizimbani leo.
 Wasanii wakiwa mahakamani.
 TID akikumbatiana na msanii Anna Kimario 'Tunda'.
Msanii wa Muziki wa kizazi kipya, Khalid Mohamed 'TID' ( wa pili kushoto), akipongezana na Johana Mathysen, baada ya maombi ya Serikali ya kuwataka kuwaweka chini ya uangalizi maalum wa miaka mitatu ili kujirekebisha tabia kutolewa uamuzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Wengine ni Romeo Bangura 'Romijons' na Anna Kimario 'Tunda'. 

Na Mwandishi wetu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia kwa dhamana wasanii 13 katika sakata la kutumia dawa za kulevya, huku ikiwaweka chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi.

Kwa pamoja wasanii hao, walifikishwa kwenye viwanja vya mahakama hiyo saa 10:00 asubuhi, huku wakiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.

Katika viwanja vya mahakama hiyo, vilitawaliwa na idadi kubwa ya watu wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki waliofika tangu saa moja asubuhi kwa ajili ya kushuhudia ndugu zao wanavyofikishwa mahakamani.

Hata hivyo, baadhi ya watu walisikika wakilalamika kutokana na kutomuona aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2006, muigizaji wa filamu Wema Sepetu.

Wasanii hao 13, waligawanywa kwenye makundi mawili ambapo la kwanza lilikuwa na wasanii nane na la pili wasanii wanne kisha kupandishwa kizimbani kwa mahakimu wawili tofauti.

Kundi la kwanza la wasanii nane wanaotetewa na wakili wa kujitegemea, Albert Msando, lilipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Kundi hilo la kwanza linamjumuisha  Hamidu Chambuso (Dogo Hamidu), Rajabu Salum, Romeo Bangura (Romijous), Cedou Madigo, Khalid Mohammed (T.I.D), Johana Mathysen, Rechoel Josephat (Recho Kizungu zungu) na Anna Kimaro (Tunda).

Mbele ya Hakimu Shaidi, wakili wa Serikali Nassoro Katuga alidai kuwa upande wa Jamhuri unawasilisha maombi yenye vipengele vitatu chini ya kifungu cha 73 (e) cha sheria ya makosa ya jinai.

Alieleza kuwa katika maombi hayo matatu ambayo yameambatanishwa na hati ya kiapo cha Ofisa Mkuu Msimamizi wa Kitengo cha Kupambana na Matumizi ya dawa za kulevya Kituo Kikuu cha Kati, Denis Mujumba.

Alidai kuwa ombi la kwanza ni kuwa mahakama iwaamuru wajibu maombi kuwa na tabia njema wakisimamiwa na wadhamini wao kwa kipindi cha miaka mitatu.

Pia mahakama iwaamuru wajibu maombi hayo kuwa wanaripoti kituo cha Polisi cha Kati mara mbili kwa mwezi ili kuangaliwa mwenendo wa tabia zao.

Mbali na hilo, pia maombi ya pili ni kuwa liwe jukumu la mahakama kuangalia itatua masharti gani yoyote dhidi ya wajibuji hao.

Wakili Katuga alidai kuwa ndani ya hati ya kiapo cha Mujumba ameeleza kuwa, akiwa kama Askari Polisi ambaye pia ni mplelelezi wa makosa ya jinai wilaya ya Ilala.

Anaeleza kuwa wajibu maombi ni wakazi wa Dar es Salaam, hivyo akiwa kama Mkuu wa kitengo cha upelelezi ana taarifa za kina kuhusu wajibu maombi hao na wenzake kujihusisha na dawa hizo za kulevya.

Hivyo kutokana na tabia hiyo endapo wakiachwa bila kuwa chini ya uangalizi uenda wakasababisha uvunjifu wa amani. Hivyo anaiomba mahakama kupokea hati hiyo ya kiapo ikiwa na maombi hayo.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Albert Msando alipinga hoja hizo na kueleza kuwa kiapo hicho kina upungufu kwa kuwa kinawazungumzia wajibu maombi kwa ujumla na bila kueleza ni taarifa zipi, zimepatikana wapi kwa nani na lini.

Alieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia wajibu maombi hayo kujua kwamba wanahusika vipi katika maombi hayo hadi kufikishwa kizimbani.

Pia kuhusu suala la uangalizi, alidai kuwa inatambulika kuwa ni kweli dawa za kulevya ni hatari lakini si vyema kwa wajibu maombi hao kuripoti kituo cha polisi kwa mwezi mara mbili ama kuwa chini ya uangalizi kwani hilo ni jukumu la Jeshi la Polisi.
Baada ya kuwepo kwa mvutano huo, Hakimu Shaidi alitoa uamuzi wake na kusema kuwa wajibu maombi hao watakuwa chini ya uangalizi chini wa mwaka mmoja ya kifungu 73 (e) na 74 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Pia watajidhamini wenyewe kwa bondi ya Sh.milioni 10 kwa kila mmoja pamoja na kuripoti kituo cha kati cha polisi kwa mwezi mara mbili.

Hakimu wa pili
Wajibu maombi wengine ambao ni Ahmed Hashim (Petiti man), Said Masoud (Said Alteza), Nassor Nassoro, Bakari Mohamed na Lulu Chelangwa (Luludiva) walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Wakili wa serikali, Katuga akishirikiana na Elia Athanas alidai kuwa upande wa jamhuri umewasilisha maombi  chini ya kifungu 73 (e) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Wakili Katuga aliyaeleza maombi hayo ambayo awali aliyasoma kwa Hakimu Shaidi wakati kundi la wasanii nane walipopandishwa kizimbani.

Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Wakili Msando alieleza kuwa wanakubaliana na maombi ya upande wa jamhuri, isipokuwa wanapinga suala la wajibu maombi kuripoti kituo cha Polisi cha Kati.

Hivyo katika uamuzi wake Hakimu Mkeha alisema kuwa mahakama hiyo imeyapokea maombi hayo ya Jamhuri na kukubaliana nayo.

Alisema kutokana na maombi hayo yalivyowasilishwa, wajibu maombi hao watakuwa chini ya uangalizi kwa miaka mitatu, pia wataripoti kwenye kituo kikuu cha polisi mara mbili kwa mwezi pamoja na kujidhamini wenyewe kwa Bondi ya Sh.milioni 20 pamoja na mdhamini mmoja atakayesaini bondi hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages