HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 07, 2017

Serengeti Boys inahitaji Bil. 1

Ni gharama za kushiriki fainali za Afrika kwa vijana Gabon
  • Malinzi aomba sapoti, alia na siasa za Uchaguzi Mkuu TFF

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amewataka Watanzania, Serikali na wadau wa michezo kuungana kufanikisha ushiriki wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ katika fainali za Afrika, inakohitaji zaidi ya Sh. Bilioni 1.

Kikosi cha Srengeti Boys kimefanikiwa kufuzu fainali hizo zinazofanyika Mei mwaka huu, baada ya kushinda rufaa, iliyokata kulalamika kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuwa Congo-Brazzaville iliyowang’oa, ilimtumia mchezaji kijeba Langa Lesse Bercy.

Serengeti Boys imepangwa Kundi B la michuano hiyo ambayo itashirikisha timu nane, zilizopangwa katika makundi mawili, ambako Tanzania imepangwa na timu za Mali, Angola na Niger, katika fainali zitakazofanyika nchini Gabon.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Malinzi alisema yeye kama Rais wa TFF ataongoza mchakato wa kupata fedha kufanikisha ushiriki wa Serengeti Boys, hata ikilazimika kujinyima zaidi ya sasa miongoni mwa watendaji wake, ili kupata kiasi hicho.

Alitia wito kwa Serikali na wadau kuisapoti Serengeti Boys ambayo haina mdhamini, huku akiainisha vyanzo vya mapato wanavyotarajia kuvitumia kukusanya sehemu ya kiasi hicho kuwa ni Ruzuku kutoka Fifa na mgawo wao wa viingilio vya mechi za Ligi Kuu.

“Zinahitajika zaidi ya Sh. Bilioni 1, ni jukumu la kila Mtanzania kusaidia upatikanaji wake. Sisi kama TFF tutajinyima zaidi ya awali, hasa ukizingatia msafara utakuwa na watu zaidi ya 40, idadi ambayo ni zaidi ya inayogharamiwa na CAF kwa malazi,” alisema.

Malinzi alifafanua kwamba, CAF inabeba gharama za watu 30 (wachezaji 23 na viongozi saba), lakini wao watakwenda Gabon na msafara si chini ya watu 40, ambao kila mmoja miongoni mwaao ana umhimu mkubwa katika ushiriki wa timu hiyo.

Kim Poulsen aipongeza TFF, Tenga

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa Serengeti Boys, Kim Poulsen, aliipongeza TFF na Kamati ya Soka la Vijana kwa upambanaji uliofanikisha ushindi kupitia rufaa iliyokatwa baada ya wapinzani kuchezesha mchezaji aliyezidi umri.

Poulsen alienda mbali kwa kumshukuru Rais wa zamani wa TFF, Leodeger Tenga, kwa msukumo mkubwa ndani ya CAF, uliowezesha kufanyiwa kazi, tena kwa haki kwa rufaa hiyo na kwamba yeye kama bosi wa ufundi, amejipanga kutowaangusha.

“Haki imetemdeka na lazima tutumie fursa hii kuwapongeza waliowezesha upatikanaji wa haki hiyo. Tumejipanga kufanya vema katika fainali, nay ale tuliyofanya katika michuano tuliyoalikwa India mwaka jana, tutayafanya Gabon,” alisema Poulsen.

Poulsen alikiri kuwa wamezidiwa ubora wa wapinzani wao kundi, ambao wamebebwa na ushiriki wao wa fainali za vijana, lakini anaamini katika ubora wa sasa wa timu yake, akiamini ina ubora utakaoweza kuwapa jeuri ya kufanya makubwa Gabon.

Siasa za Uchaguzi Mkuu zamtesa Malinzi

Katika hatua nyingine, Rais Malinzi amezikana tuhuma zinazosambaa kuwa kiasi cha Sh. Bil. 1.5 kimetoweka katika akaunti za TFF kwa njia za panya, na kusema hizo ni siasa za majitaka kuelekea Uchaguzi Mkuu wa TFF, mwisho wa mwaka huu.

Malinzi alibainisha ya kwamba, tangu akiwa Libreville, nchini Gabon, amekuwa akizisikia tuhuma hizo, alizowataka Watanzania kuzipuuza, kwani hazina ukweli wowote, zaidi ya makundi ya wanaotamani kushika hatamu za uongozi TFF.

“Kiasi kinachosemwa kuwa kimetoweka, ni kile cha Dola 550,000 kutoka Fifa, ambazo mwaka jana 2016 hazikutolewa na shirikisho hilo la kimataifa, baada ya kufuta miradi mbili ya Fifa Goal Project na Fifa Football Development.

“Fifa imeifuta miradi hiyo mwaka jana, hivyo haikutoa fedha kama ilivyo miaka mingine. Bahati nzuri mimi ni Mjumbe Kamati ya Maendeleo ya Fifa, fedha hizo zikitoka nitajua na zitatumika kwa mipango stahili, haziwezi kuibwa,” alisisitiza Malinzi.

Aliwataka wanamichezo wanaotaka kuwania uomgozi katika uchaguzi ujao wa TFF, kusubiri muda wa kampeni, watoe sera na kisha kuchaguliwa, na sio kuunda tuhuma zenye mlengo wa kuwaharibia walio madarakani kwa sasa.

“Kama wewe unataka kugombea moja ya nafasi TFF, ama una mtu ambaye ungependa awe kiongozi, kuweni wastaarabu. Awali walituzushia kuwa tunataka kupunguza idadi ya wapiga kura kwa maslahi yetu, wakati sio,” alisisitiza.

Malinzi alibainisha ya kwamba, punguzo la wajumbe wa Mkutano Mkuu, halikuwa wazo wazo lake yeye wala kiongozi yeyote ndani ya TFF, bali lilitokana na matakwa ya kisheria ya Fifa, na wao kama wahusika waliliwasilisha kwa nia njema.

 Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu maandalizi ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ katika mashindano ya Afrika kwa vijana. (Picha na Francis Dande).  

 Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu maandalizi ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ katika mashindano ya Afrika kwa vijana. 

No comments:

Post a Comment

Pages