Husna Saidi na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
MWANARIADHA wa zamani wa Kimataifa, Juma Ikangaa anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya riadha ya Dasani Marathon yanayotarajia kufanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Mei mwaka huu.
Mashindano hayo ya umbali wa kilometa 10 na 21 yanatarajia kushirikisha zaidi ya wanariadha 1000 kutoka Mikoa mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Coca Cola Kwanza, Nalaka Hettiarachchi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mashindano hayo yaliyolenga kukuza mchezo wa riadha na kujenga afya kwa wanamichezo.
Hettiarachchi alisema kuwa wameamua kudhamini shindano hilo kama njia moja wapo ya kushiriki katika shughuli za kijamii pia kwa sababu lina lengo la kukuza vipaji vya wanariadha wa Tanzania ili kuwawezesha kutamba katika mashindano ya Kimataifa.
“Mashindano haya yatadhaminiwa na kampuni ya Coca Cola kwanza kupitia kinywaji chetu cha maji ya dasani, ambapo wakati wa kukimbia wanariadha watakuwa na wakati wa kupata maji ya kupoza koo” alisema Hettiarachchi.
Kwa upande wake Rais wa Chama Cha Wakimbiaji Mkoa wa Dar es Salaam , Goodluck Elvis alisema mashindano hayo yatashirikisha wakimbiaji wa wanaume na wanawake wa rika tofauti na washindi watajipatia zawadi za fedha taslimu pamoja na medali kwa watakaomaliza mbio.
“Mbio hizo za kilomita 10 na kilomita 21 zitakazoanzia na kuishia katika bwalo la Maofisa wa Polisi - Masaki usajili wake unaendelea kufanyika katika maeneo ya Colosseum Gym, Masaki, Shoppers Supermarket, Mikocheni na Mlimani City Mall,” alisema Elvis.
Aidha, alifafanua kuwa gharama za usajili kwa ajili mashindano hayo ni Tsh. 30,000 kwa kila mshiriki ambapo mshiriki atapatiwa begi na fulana kwa ajili ya kushiriki katika mashindano hayo.
Mashindano hayo yameanzishwa miaka mitatu iliyopita na yameendelea kufanya vizuri mwaka hadi mwaka, Kampuni ya Cocacola inategemea kutoa ufadhili katika mashindano hayo kwa zaidi ya miaka mitano ijayo.
No comments:
Post a Comment