Naibu Waziri wa Elimu Mhandisi Stella Manyanya amemuagiza
msimamizi wa ukarabati wa shule ya Sekondari Kantalamba kuhakikisha kuwa walemavu
wanajengewa vyoo vyao ndani ya mabweni wanamolalia nia ikiwa ni kujiepusha na
kuwaamsha wenzao usiku pindi wanapotaka kwenda chooni.Ametoa agizo hilo leo jumapili (30/7/2017) muda mfupi baada
ya kufanya ukaguzi wa ukarabati wa shule hiyo iliyopo Wilayani Sumbawanga iliyopewa
Shilingi Bilioni 1.1 ikiwa ni mpango wa serikali wa kuzirudishia hadhi shule
kongwe nchini huku shule hiyo ikiwa ni ya tangu 1964.
“Lazima muhakikishe kwamba Mnakuwa na vyumba maalum kwaajili
ya wanafunzi wenye ulemavu na kuwawekea miundombinu hasa kwa wale walemavu
ambao mazingira yao ni magumu Zaidi, kwa mfano mwanafunzi ana ulemavu wa miguu
na anatakiwa kwenda chooni hapaswi kutambaa kwenye mikojo ya wanafunzi wenziwe
hii inawapelea wao kuwa katika mazingira hatarishi zaidi,” Alisema.
Mbali na agizo hilo pia Mhandisi Manyanya ametoa wiki tatu ukarabati
wa shule hiyo kumalizika baaada ya muda waliopangiwa kumalizika huku
kipaumebele kikiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo yao katika
hali ya utulivu.
“Sijaridhishwa na kasi ya ukarabati huu hivyo tumewaongezea
wiki tatu mhakikishe mnamaliza ili wanafunzi waendelee na masomo maana yake
kama mngekuwa hamwezi kumaliza kwa wakati kwanini msingesema mapema,” Alisisitiza.
Aidha alipokuwa anakagua bwalo la kulia wanafunzi aliagiza
kutanuliwa kwa bwalo hilo baada ya kuona kuwa bwalo hilo ni dogo na wanafunzi
ni wengi kiasi ambacho ingewabidi wanafunzi hao kula kwa zamu ili wote waweze
kulitumia bwalo hilo na kuongeza kuwa ukarabati unaofanyika ni pamoja na
utanuzi wa majengo kwani ukubwa wa jengo lililopo ni wa tangu 1964 na sasa ni
2017.
Kabla ya kumaliza ziara yake shuleni hapo aliwasisitizia
wanafunzi kuwa nia ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kuwa hakuna tofauti
kati ya shule za serikali na shule binafsi kuanzia huduma za majengo, elimu na
vifaa vya kusomea.
IMETOLEWA NA
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA
E-mail: ras@rukwa.go.tz
No comments:
Post a Comment