HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 31, 2017

YALIYOJILI KIKAO CHA KAMATI YA UTENDAJI TFF

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, imekutana Jumapili Julai 30, 2017 katika Ukumbi wa Hosteli za TFF, zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam yaliko Makao Makuu ya shirikisho.

Kikao hicho, kimepitisha mambo mbalimbali ambako miongoni mwake ni mabadiliko ya Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Miongoni mwa kanuni ziliguswa ni ya kuhusiana  na kujali afya za wachezaji pamoja na mikataba wanayoingia na klabu.

Hivyo, TFF imeagiza msimu wa 2017/18 mchezaji atayesajiliwa hatapewa leseni ya kumruhusu kucheza mashindano husika kama vile Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL), Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kama hatakamilisha masharti makuu matatu kwa mujibu wa kanuni.

Masharti hayo ni kukatiwa Bima ya Matibabu, Kuidhinishwa afya yake ambayo mara baada ya fomu yake kupitishwa na Kamati ya Tiba ya TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 18 (1) ya Ligi Kuu na Mkataba wake wa maandishi ‘hardcopy’ kuwasilisha TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 69 (8) ya Ligi Kuu.

Kama kuna timu haitakidhi japo sharti moja kati ya hayo, basi mchezaji wake hatapewa leseni ya kucheza kwa msimu husika. Kaimu Rais wa TFF, Wallace Karia, akifunga hoja hiyo, alisisitiza akisema: “Wakati huu hatutaki siasa. Tusimamie kanuni hizi, hatutaki kuleta mchezo msimu huu.”

Hayo yamekuja baada ya klabu kutakiwa kuwawekea Bima ya Matibabu kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1) inayosema: “Kila Klabu ina wajibu wa kuwawekea wachezaji wake bima ya matibabu na fidia kutokana na ajali michezoni. Klabu itakayokiuka kanuni hii itakuwa imepoteza sifa ya kuwa klabu ya Ligi Kuu, na usajili wa wachezaji wa timu yake hautathibitishwa na haitashirikishwa katika Ligi Kuu.

Kuhusu Mikataba kwa mujibu wa Kanuni ya 69 (8), Kamati ya Utendaji imekubaliana kwamba: “Mikataba yote ya wachezaji ambao haujasajiliwa na kuthibitishwa na TFF, hautatambuliwa.”

Kadhalika, kuhusu wachezaji wa Kigeni kwa mujibu wa Kanuni ya 57 (5), kitasomeka kama ifuatavyo: “Mchezaji ye yote wa kigeni anayesajiliwa katika Ligi Kuu atalipiwa ada maalumu ya Sh milioni mbili (Sh 2,000,000) kwa msimu kwa mchezaji mmoja ili usajili wake uweze kuthibitishwa na kuruhusiwa kucheza.

Gharama za awali zilikuwa ni dola 2,000 za Marekani (sawa na Sh. 4.5 milioni.) kwa mchezaji mmoja. 

Kadhalika, sasa kwa mujibu wa kanuni ya 13 (6) Klabu Mwenyeji itakuwa na nafasi ya kuweka mpaka mabango 10 ya Mdhamini/Wadhamini wake. Ukubwa wa bango moja lile lenye vipimo vya 6m x 1m. 

Kama timu ni mgeni katika mchezo husika, ana uwezo kufanya makubaliano na mwenyeji wake akampa nafasi katika hayo 10 ambayo yameruhusiwa kikanuni.

Aidha, Kanuni ya 14 imeongezwa kipengele kimoja. Kanuni ya 14 (48) Klabu ina wajibu wa kushirikiana na mdhamini wa matangazo ya televisheni ikiwemo kupata picha za wachezaji na benchi la ufundi kwa ajili ya maandalizi ya mechi zao.

Na Kanuni 14 (49), inasema: TFF/TPLB itachukua hatua kwa ukiukwaji wo wote wa taratibu za mchezo kama zilivyoanishwa kwenye Kanuni ya 14 kwa kutoa onyo kali au karipio au kutoza faini kuanzia Sh. 200,000 (lakini mbili) mpaka Sh. 300,000 (laki tatu), na/au kufungia mchezo isiyozidi mitatu (3) au kipindi kisichozidi miezi mitatu (3) kwa mchezaji, kiongozi au timu.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Utendaji imeridhishwa na maandalizi ya Mkutano Mkuu ujao wa TFF ambako pamoja na mambo mengine utakuwa na ajenda ya Uchaguzi Mkuu wa shirikisho unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.

Mjumbe wa FIFA, Solomon Mudege alikuwa nchini kwa siku ya Jumamosi ambako alipata fursa ya kuzungumza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe; Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yussuph Singo pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF wakiongozwa na Kaimu Rais Wallace Karia.

Mara baada ya kupata maelezo ya kuridhisha kutoka kwa wanafamilia hao wa mpira wa miguu ambao baadhi yao alikutaa nao mmoja baada ya mwingine, alibariki mchakato wa uchaguzi uendelee na Kamati ya Utendaji imetangaza kuwa utafanyika Ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma.

Mudege alikuwa nchini kuangalia hali maendeleo ya mpira wa miguu nchini hasa katika utawala, lakini kwa kuwa uongozi uliokaimu madaraka umefuata taratibu, kanuni na sheria tangu mwanzo, mjumbe huyo aliridhia mchakato wa uchaguzi na shughuli nyingine ziendelee kama zilivyopangwa.

MATOKEO YA MWISHO USAILI TAFCA, KAMPENI ZAANZA

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA), Ramadhani Mambosasa ametangaza orodha ya majina sita ya mwisho ya wagombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.

Kwa mujibu Mambosasa, wagombea hao kwa sasa hawana budi kuendelea na kampeni hadi Agosti 9, mwaka huu ambako uchaguzi huo umepangwa kufanyika kufanyika Agosti 10, mwaka huu mjini Dodoma.

Waliopitishwa katika orodha ya mwisho kuwania nafasi mbalimbali za uongozi - ngazi ya taifa ni pamoja na Kidao Wilfred, Lister Manyara, Michael Bundala, Dismas Haonga, Jamhuri Kihwelo, George Komba, Samuel Moja na Maka Mwalwasi na Mohammed Tajdin.

Nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Wajumbe wa Mkutano Mkuu TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
……………………………………………………………..………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages