Mkazi wa
kijiji cha Shiponga, Hanang Mkoani Manyara anayedaiwa kuwa jambazi, Hamisi
Athumani (32), amefariki dunia baada ya kupigwa risasi kiunoni na askari polisi
wakati akiwa katika harakati ya kutoroka.
Kamanda wa
Jeshi la Polisi Mkoani hapa, ACP Debora Magiligimba, amesema tukio hilo
limetokea Agosti 25 mwaka huu saa nane mchana, huko katika kijiji cha Mgori
tarafa ya Ngimu wilaya ya Singida.
Amefafanua
kuwa Hamisi (marehemu) alipigwa risasi na askari polisi wakati akijaribu
kuwatoroka mara baada kuonyesha bunduki aina ya rifle yenye namba 7358 na
risasi zake tano.
Amesema
bunduki hiyo iliyokuwa imekatwa mtutu na risasi zake tano zilikuwa zimefichwa
kwenye soksi, vitu hivyo vilikuwa vilihifadhiwa kwenye mfuko wa sandarusi, na
kufichwa chini ya jiwe.
ACP
Magiligimba amesema Agosti 23 mwaka huu, mtuhumiwa alikamatwa na wananchi wa
kijiji cha Ngamu, na kufikishwa katika kituo cha polisi cha kijiji hicho kwa
tuhuma ya kujihusisha na matukio ya ujambazi.
“Kesho yake
mtuhumiwa alihojiwa na kukiri kujihusisha na matukio ya ujambazi wa kutumia
silaha katika mikoa mbalimbali. Pia aliahidi kuwapeleka askari kuwaonyesha
mahali alikoificha silaha anayoitumia kwenye matukio hayo ya ujambazi”, amesema
ACP Magiligimba.
Kamanda huyo
amesema Agosti 25 mwaka huu saa sita mchana, askari polisi wakiwa na mtuhumiwa,
walikwenda katika pori la kijiji cha Mgori mahali alipokuwa ameficha bunduki
hiyo aina ya rifle.
“Mara tu baada
ya kuwaonyesha askari hao silaha hiyo na wakati askari wanaendelea kufanya
upekuzi katika eneo hilo, mtuhumiwa alijaribu kutoroka askari kwa kukimbia” amesema
na kuongeza;
“Askari mmoja
alifyatua risasi tatu hewani akimtaka asimame, lakini hakutii. Ndipo alipompiga
risasi moja iliyompata sehemu ya kiunoni”.
Amesema jereha
hilo la risasi lilisababisha mtuhumiwa Hamisi avuje damu nyingi, na hivyo
kufariki dunia wakati akikimbizwa hospitali ya mkoa kwa matibabu.
“Jeshi la
Polisi Mkoa wa Singida linaendelea kutoa wito kwa wananchi waote kutoa taarifa
zitakazosaidia kubaini wahalifu katika maeneo yao ili hatua ziweze kuchukuliwa
kudhibiti vitendo vya kihalifu”, amesema kamanda huyo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba akionyesha bunduki aina ya rifle iliyokuwa ikimilikiwa na mtuhumiwa wa ujambazi Hamisi Athumani (32) mkazi wa Shiponga-Hanang mkoa wa Manyara anayedaiwa kuitumia kwenye matukio ya ujambazi. (Picha/habari na Nathaniel Limu).
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba akionyesha bunduki aina ya rifle iliyokuwa ikimilikiwa na mtuhumiwa wa ujambazi Hamisi Athumani (32) mkazi wa Shiponga-Hanang mkoa wa Manyara anayedaiwa kuitumia kwenye matukio ya ujambazi. (Picha/habari na Nathaniel Limu).
No comments:
Post a Comment