HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 31, 2017

TFF YATANGAZA VIINGILIO, MSUVA ATUA STARS

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya mchezo kati ya Taifa Stars ya Tanzania na Botswana utakaofanyika Jumamosi Septemba 2, mwaka huu.

Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam chini ya utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) viingilio vitakuwa Sh 10,000 kwa Jukwaa Kuu na Sh 5,000 kwa mzunguko.

Wakati huo huo, Kiungo Taifa Stars, Simon Msuva tayari amejiunga na timu hiyo akitokea Klabu ya Difaa El Jadidah ya Morocco baada ya Shirikisho la Soka Morocco na timu yake kumfanyia mpango wa visa ya muda mrefu iliyomwezesha kusafiri.

Mchezaji ambaye imeshindikana kuja ni Orgenes Mollel wa FC Famalicao ya Ureno. Sababu ni taratibu za ruhusa za kimataifa zinafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria za nchi ya Ureno ambako anacheza soka la kulipwa.

Nyota wengine walikwisha kuripoti ni pamoja na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Elias Maguli (Dhofar FC/Oman), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya) wakati Farid Mussa wa CD Tenerif ya Hispania anatarajiwa kutua leo.

Wengine ambao wako kambini Hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).

Pia wamo Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).

Viungo ni Himid Mao - Nahodha Msaidizi (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Shiza Kichuya (Simba SC), wakati Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans), Kelvin Sabato (Azam FC) na Emmanuel Martin (Young Africans).

Katika hatua nyingine, Botswana inatarajiwa kuingia usiku wa saa 3.00 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) na watafikia Hoteli ya Urban Rose iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Botswana inayonolewa na David Bright inakuja na wachezaji 18 wakiwamo makipa Mampule masule, Noah Maposa na Antony Gouws.

Walinzi ni Letsweletse, Mosha Gaolaolwe, Simisane Mathumo, Thabang Mosigi, Lesenya Ramorake, Tapiwa Gadibolae na Bokani Leeton.

Viungo ni Alphonse Modisaotsile, Maano Ditshupo, Katlego Masole, Gift Moyo, Segolame Boy, Lemponye Tshireletso, Thero Setsile, Kabelo Seakanyeng,Jackson, Lemogang maswena.

Washambuliaji ni Tumisang Orebonye, Jarome Ramathakwane, Tebogo Sembowa, Hendric Moyo na Boipelo Oaitse.


KIDAO AZUNGUMZIA RATIBA VPL

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kidao Wilfred ameunda kikosi kazi cha wataalamu wanne wa shirikisho kuangalia upya ratiba ya Ligi Kuu ili kuondoa kila aina ya kero inayoweza kuibuka katikati ya mashindano.

Kidao ambaye ana siku tisa ofisini tangu ashike wadhifa huo, amesema kuna changamoto nyingi sana katika shirikisho, lakini kubwa ni hili ambalo wanafamilia ya mpira wa miguu wamekuwa wakijadili kwa sasa.

Wadau wanajadili suala la ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kwamba baada ya michezo ya mzunguko wa kwanza tu, ratiba imetangazwa kubadilishwa. Ni kweli imebadilishwa kwa sababu ya kupisha wiki ya kalenda ya FIFA ya mechi ama za ushindani au kirafiki kati ya nchi na nchi.

Amesema kwamba makosa yamefanywa na maofisa wa Bodi ya Ligi Kuu ambayo ndiyo yenye dhamana ya kupanga ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL).

Maofisa hao ilihali wakijua kwamba kuna wiki ya kalenda ya FIFA, walidiriki kupanga mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Sasa tuchukua nafasi hii kuomba radhi Watanzania hususani wanafamilia ya mpira wa miguu ambao kwa namna moja au nyingine wameghafirishwa na kupanguliwa ratiba.

“Lakini suala hili haliwezi kupita hivi hivi bila hatua na kinidhamu kuchukuliwa. Rais wa TFF Bw. Wallace Karia aliniagiza nimwandikie Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Bw. Boniface Wambura achukue hatua za kinidhamu kwa maofisa wote waliohusika na upangaji huo wa ratiba ulioingilia ratiba ya kalenda ya wiki ya FIFA,” amesema Kidao.

Hatua hizi za kinidhamu si kwa kupanga mechi wakati wa Wiki ya FIFA pekee, bali maofisa hao wamehusika kupanga ratiba ambayo tathmini ya uongozi imeonyesha kwamba si rafiki kwa timu zote 16 zinazoshiriki VPL.

Hii ni kwa sababu kuna baadhi ya timu zimepangiwa kucheza mechi nyingi nyumbani au ugenini wakati wa kumaliza Ligi Kuu hasa duru la pili linaloanzia Desemba, 2017 hadi Mei, 2018.

Ikumbukwe tu kwamba ratiba hii ilipangwa kabla ya uongozi wa Rais Wallace Karia na Kamati nzima ya Utendaji kuchaguliwa katika wadhifa huo.

“Ninachotaka kusema  hapa ni kwamba, Kamati ya Utendaji iliyoingia madarakani Agosti 12, mwaka huu iliona upungufu na hivyo kuagizwa ratiba ipangwe upya kwa kuzingatia uwiano wa michezo ya ugenini na nyumbani ili kwa namna moja au nyingine kusiwe angalau na hisia za kupanga matokeo,” amesisitiza.

Vita ya upangaji wa matokeo ni kubwa sana ambayo FIFA wamekuwa wakihubiri na kuagiza mashirikisho katika mabara yote kadhalika mashirikisho ya nchi kupiga vita upangwaji wa matokeo.

Kidao amezungumza hayo baada ya kukutana na wanahabari kwa mara ya kwanza tangu kueuliwa kushika wadhifa wa Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).


UAMUZI WA KAMATI YA NIDHAMU

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), chini ya Makamu Mwenyekiti, Peter Hellar ilikutana jana Jumatano Agosti 30, mwaka huu ikiwa na ajenda kuu ya mashauri yanayohusu wachezaji watatu.

Wachezaji hao ni Obrey Chirwa wa Young Africans pamoja na wenzake wawili Deus Kaseke na Simon Msuva ambao kwa pamoja msimu uliopita walikuwa wanaitumikia klabu hiyo ya Jangwani.

Wachezaji hao walisimamishwa kucheza soka katika uamuzi uliofanywa na Kamati ya 72 ya Bodi ya Ligi kwa mujibu wa kanuni ya 9 (5) ya Ligi Kuu kutokana na kumvamia na kumsukuma mwamuzi Ludovic Charles aliyechezesha mechi ya Young Africans na Mbao Mei 20, mwaka huu.

Kati ya watuhumiwa wote, Kamati ilimtia hatiani Simon Msuva na kuwaachai huru Deus Kaseke na Obrey Chiwa. Msuva alionekana kumvamia na kumwangusha mwamuzi kinyume cha kanuni ya 49 (1) (b) ambako sasa anatakiwa kusimama mechi tatu za aina yo yote ya mashindano ya ndani.

Kwa mujibu wa Wakili Hellar tayari Msuva alikosa mechi za mashindano ya Sportpesa hivyo Kamati imetambua kwamba tayari ametumikia adhabu husika, lakini inampa onyo kali la maandishi kwa mujibu wa kanuni ya 14.

Kamati imeshauri TFF na Bodi ya Ligi ni vema kuachia Kamati majukumu ya kusimamisha na kufungia kwa mujibu wa kanuni za kinidhamu badala ya taasisi hizo kuchukua hatua ya kusimamisha ambazo hazileti haki na usawa uwa ni kama adhabu.

Ushauri huo umepokelewa na TFF na itaufanyia kazi.

Itakumbukwa kwamba mechi iliyowaletea shida wachezaji hao ni namba 236 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Yanga ikipoteza kwa bao 1-0.

Mara baada ya mchezo huo, Kamati ya 72 ya Bodi ya Ligi ilipitia matukio mbalimbali na kufikia uamuzi wa kuwasimamisha wachezaji Deus Kaseke, Simon Msuva na Obrey Chirwa wa Yanga kucheza mechi za Ligi Kuu.

Walisimamishwa wakisubiri suala lao la kumsukuma na kumwangusha Mwamuzi Ludovic Charles kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Wachezaji hao walidaiwa kufanya kitendo hicho katika mechi hiyo dhidi ya Mbao FC iliyofanyika Mei 20, 2017 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijni Mwanza. Uamuzi wa Kamati ya Saa 72 ulizingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.

Itakumbukwa, Mwamuzi Ludovic Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo. Uamuzi dhidi yake ni kwa mujibu w Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.


……………………………………………………………………..……………..……
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages