Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Gladys Bejarano katika Mji wa Havana nchini Cuba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Bi. Gladys
Bejarano na kumuhakikishia ufunguzi wa ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini
humo.
Amesema Tanzania inayatambua na kuyathamini mahusiano mazuri ya
kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi, kielimu, kiafya na kiutamaduni kati yake na
Cuba, hivyo inatarajia kufungua ubalozi nchini humo ili kurahisisha utendaji wa
kazi za kibalozi.
Waziri
Mkuu alikutana na Bi. Gladys jana jioni (Jumamosi, Agosti 26, 2017) wakati
alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi nchini Cuba. Malengo ya ziara yalikuwa ni kuimarisha na kudumisha ushirikiano
kati ya nchi hizo mbili.
“Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati Tanzania na Cuba,
ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba
wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere, hivyo lazima tufungue ofisi za ubalozi na
tutamleta balozi wetu hapa.”
Pia Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Cuba kwa ujenzi wa
kiwanda cha dawa za kuulia vijidudu vya maralia pamoja na ufadhili wa masomo ya
udaktari inaoutoa kwa wanafunzi wa Kitanzania ambao wanasoma katika vyuo
mbalimbali nchini humo.
Hata hivyo aliiomba Serikali hiyo iendelee kutoa ufadhili wa
masomo kwa madaktari hao hadi ngazi ya shahada ya uzamili kwa sababu Serikali
ya Tanzania inawahitaji madaktari bingwa wengi kwani walioko nchini ni
wachache.
Kwa upande wake, Bi. Gladys
alimshukuru Waziri Mkuu kwa kufanya ziara nchini Cuba na alimuhakikishia kwamba
uhusiano wa Serikali yake na Serikali ya Tanzania utaendelea kuimarishwa kwa manufaa
ya wananchi wa pande zote mbili.
Alisema Serikali ya Tanzania
chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha
uchumi wake unakua kwa kasi jambo ambalo ni tofauti na mataifa mengine. “Nawapongeza
kwa hatua za kimaendeleo mnazozifanya.”
Makamu huyo wa Rais
alisema Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji
wa Sekta za Afya, Utamaduni, Kilimo, Uchumi na Elimu. Kuhusu ombi la kuongeza
ufadhili wa shahada ya uzamili kwa madaktari alisema amelipokea na atalifanyia kazi.
Awali Balozi wa
Tanzania nchini Canada, ambaye anasimamia na nchi ya Cuba, Balozi Jack Zoka
alisema Serikali ya Cuba ni miongoni mwa nchi zinazoshirikiana na Tanzania
katika uboreshaji wa shughuli za maedndeleo, hivyo uwepo wa ofisi za ubalozi
nchini humo utazidi kuimarisha mahusiano.
No comments:
Post a Comment