BENKI ya NMB
imezindua huduma mpya ya ‘NMB
Pamoja Account’ na NMB Chap Chap kwa
ajili ya kusaidia vikundi vya wajasiriamali na VIKOBA hapa nchini.
Kuzinduliwa kwa huduma hiyo kumeenda sambamba na benki hiyo
kuingia ubia na Umoja wa Vikundi vya vikoba nchini (VIGUTA) ili kuvihudumia
vikundi hivyo vyote vilivyopo nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika uzinduzi huo,
Mkurugenzi wa NMB, Ineke Bussemaker alisema lengo la kufanya hivyo ni
kuhakikisha wana vikundi wanatunza fedha zao katika sehemu iliyo salama na
kuwawezesha kujiimarisha kibiashara zaidi.
Alisema zama za zamani za kuweka fedha za vikoba kwa mtu
zimepitwa na wakati na ndio sababu benki ya NMB ikabuni uwekaji wa fedha kwao
na kuwaunganisha pamoja.
Bussemaker alisema kwa mwaka huu, NMB inatarajia kufikia
lengo la kuwa na vikundi vilivyojiunga kwao visivyopungua 18,400.
Naye Mkurugenzi wa Mtendaji wa Muungano wa Vikoba nchini
(VIGUTA), Dk. Salmin Dauda alisema wanajivunia kuungana na NMB huku wakiwa na
wanachama milioni 7.2 na zaidi ya
vikundi 92,000 ambao wanaweza kutumia benki hiyo wakiwa popote nchini.
Alisema wanaamini kupitia VIGUTA na muungano wa NMB
itawasaidia kupata mikopo na kukuza biashara zao itakayowasaidia kuwaondoa
katika dimbwi la umaskini.
Benki ya NMB hadi sasa ina matawi 200 na wateja mil 2.5
nchi nzima na inatoa huduma mbalimbali za kifedha ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment