Na Beatrice Lyimo- MAELEZO DODOMA
Serikali imepanga kuongeza idadi ya Maafisa Ugani wenye ujuzi katika kila Kata na Kijiji ili kuleta mapinduzi ya kilimo Nchini.
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. William Ole
Nasha wakati akijibu swali lililohusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha
inafanya mapinduzi ya kilimo kwa kuwa na wataalamu wa kutosha, leo
Bungeni mjini Dodoma.
Naibu Waziri huyo amesema
kuwa Serikali inatambua kuwa Sekta ya Kilimo ni muhimu na ndiyo yenye
kuajiri watanzania wengi hivyo mapinduzi ya kilimo yatachangiwa na uwepo
wa wataalam wa kutosha wenye taaluma na ujuzi stahiki ili waweze
kushauri matumizi ya teknolojia na kanuni bora za kilimo.
"
Hadi kufikia mwaka 2016/2017 Serikali imeajiri maafisa ugani 8,756 sawa
na asilimia 43 ya mahitaji ya maafisa ugani 20,374 katika ngazi ya
Kijiji, Kata na Wilaya" amefafanua Naibu Waziri Ole Nasha.
Aidha,
Naibu Waziri Ole Nasha aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha na
kuwezesha vituo vya kilimo na vituo vya Rasilimali za kilimo za kata
(WARCs) kwa ajili ya kufundishia teknolojia mbalimbali za kilimo.
Vilevile
alisema kuwa Serikali itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kuandaa
miongozo na mafunzo ya huduma za ugani, ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa kazi za Ugani na kuboresha usambazaji wa teknolojia za
kilimo bora kwa wakulima nchini.
Mbali na hayo Serikali inaendelea kusomesha vijana na kuwaajiri kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
No comments:
Post a Comment