HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 24, 2017

STARS KUJIPIMA NA BENIN

Kocha Mkuu Salum Mayanga, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kikosi cha wachezaji 24 kitakachopambana na Benin.

NA MAKUBURI ALLY

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Salum Mayanga ametaja kikosi cha wachezaji 24 kitakachocheza mchezo wa Kimataifa wa kirafiki dhidi ya Benin utakaochezwa Novemba 11 nchini humo.

Mayanga alisema mchezo huo uko kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA) ambako katika kikosi chake ameita wachezaji 21 wa timu mbalimbali na kuwaongeza wachezaji watatu kutoka timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20.

Mayanga alisema kambi ya timu hiyo itaanza Novemba 5 ambako itafanya mazoezi kwa siku nne kabla ya kwenda Benin kwenye mchezo huo wa Kimataifa wa kirafiki ulio kwenye kalenda ya Fifa.

Alisema mara nyingi aliomba mechi za Kimataifa za kirafiki nje ya Afrika Mashariki na kufanikiwa kuipata Benin ambayo itawasaidia kuwajenga zaidi kwa ajili ya kampeni za kuwania kufuzu kwa michuano ya Afrika (AFCON) mwakani.

“Mechi mbili zilizopita kabla ya leo (jana) nilieleza kwamba naijenga timu kuanzia safu ya beki, sasa hivi naiweka sawa kuanzia eneo la katikati kwenda mbele,” alisema Mayanga.
Aidha Mayanga alisema katika mpangilio wake aliomba mechi mbili kwa ajili y Stars, mojawapo ikiwa Msumbiji ambao walikubali lakini juzi walituma barua ya kuukacha mchezo huo kwa sababu uwanja wao una matumizi mengine.   
   
Kikosi cha Stars kinaundwa na Makipa ni Aishi Manula, Ramadhani  Kabwiili na Peter Manyika walinzi wa pembeni  ni Gadiel Michael, Erasto Nyoni na Boniface Maganga huku walinzi wa kati ni Abdi Banda, Kelvin Yondani na Nurdin Chona.

Viungo wa kati ni Himid Mao, Hamis Abdallah, Mzamiru Yassin, Raphael Daud na Mohamed Issa, viungo wa pembeni ni Simon Msuva, Shiza Kichuya, Faridi Mussa na Ibrahim Ajib, washambuliaji ni Mbwana Samatta, Mbaraka Yusuph na Elias Maguli.

Katika kikosi hicho, Mayanga amewaongeza vijana watatu wenye umri chini ya miaka 20 ambao ni Yohana Mkomola, Abdul Mohamed na Dickson Job.

No comments:

Post a Comment

Pages